1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Union Berlin yamtetea Eta dhidi ya ubaguzi

13 Aprili 2026

Union Berlin imelaani vikali maoni ya kibaguzi dhidi ya Marie‑Louise Eta, kocha wa kwanza mwanamke kuongoza timu katika ligi tano kubwa za Ulaya.

https://p.dw.com/p/5C5nw
Union Berlin | Kocha Marie-Louise Eta
Klabu imetoa ujumbe mkali huku Eta akichukua majukumu ya kocha wa muda katika juhudi za kuokoa nafasi ya Union Berlin kwenye Bundesliga.Picha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Baada ya kumteua Marie-Louise Eta kuwa kocha mkuu wa kwanza mwanamke katika ligi kuu tano kubwa barani Ulaya, klabu ya Union Berlin imesema "inasimama naye bega kwa bega” huku ikilaani maoni ya kudhalilisha wanawake yaliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii.

Mchezo wake wa kwanza kama kocha katika Bundesliga utakuwa Jumamosi dhidi ya Wolfsburg. Tayari kumekuwepo na maoni ya ukosoaji mtandaoni yakidai kwamba hafai kwa kazi hiyo kwa sababu ni mwanamke.

Akaunti ya Union Berlin kwenye X ilijibu chapisho lililodai kwamba wachezaji hawatamchukulia kwa uzito kocha mwanamke katika masuala ya mbinu za mchezo kwa kusema: "Kwa heshima yote, huo ni ubaguzi wa kijinsia.” 

Eta amekuwa sehemu ya benchi la ufundi la klabu kwa muda mrefu, akiwa msaidizi wa timu ya wanaume na pia kocha mkuu wa timu ya vijana chini ya miaka 19.

Klabu hiyo pia iliita maoni mengine "ya kibaguzi” baada ya kudai kwamba kocha mwanamume atakayefungwa na timu yake ataonekana amepoteza heshima.

Ikijibu chapisho lililoonyesha wasiwasi kuhusu jinsi Eta atakavyotendewa na uwezekano wa mashambulizi ya kijinsia endapo atapoteza mchezo, klabu ilisema: "Familia ya Union inasimama naye.”

Eta ameteuliwa kuwa kocha wa muda kwa mechi tano za mwisho za msimu huku Union ikipambana kuhakikisha inabaki Bundesliga msimu ujao. Klabu ilishasema awali kwamba msimu ujao ataiongoza timu ya wanawake kama kocha mkuu.

Uamuzi wa kumteua Eta ulipongezwa na Meya wa Berlin, Kai Wegner, aliyesema ni "ishara madhubuti kwa soka la kulipwa na kwa wanawake katika michezo ya kiwango cha juu,” ingawa aliandika jina lake vibaya. Klabu ilimsahihisha, naye akajibu: "Tulikuwa tumeshangazwa sana.”