1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Watoto 1,000 hufa kila siku kwa kunywa maji machafu

22 Machi 2023

Shirika la UNICEF limesema zaidi ya watoto 1,000 walio chini ya umri wa miaka 5 hufa kila siku ulimwenguni kote kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

https://p.dw.com/p/4Ow9u
Fischerei in Indonesien
Picha: Afriadi Hikmal/NurPhoto/imago images

Ripoti hiyo ya shirika la UNICEF iliyozinduliwa Jumatatu mjini New York, ilisema jumla ya watoto milioni 190 katika nchi 10 za Afrika wako katika hatari.

Kulingana na tathmini yao mpya, shirika hilo linasema hali ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya kati mfano Benin, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Cote d'Ivoire, Guinea, Mali, Niger, Nigeria na Somalia.

Mengi ya mataifa hayo yanakabiliwa na misukosuko ya kisiasa na machafuko ya silaha yanayofanya hali kuwa mbaya zaidi hasa kwa watoto kuweza kupata maji salama na usafi wa mazingira kuimarishwa.

Jumatano 22.03.2023, ni siku ya kimataifa ya Maji. Pia ni siku ambayo mkutano mkubwa kuhusu maji ambao umeandaliwa na Umoja wa Mataifa unaanza mjini New York. Lengo la mkutano huo ni kuchambua kiwango ambacho kimefikiwa kwenye Malengo ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo, Maendeleo Endelevu na uwezekano wa watu wote kupata maji safi ifikapo mwaka 2030.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu bilioni 2 kote ulimwenguni, hiyo ikiwa ni mtu mmoja katika kila watu wanne, hawawezi kupata maji safi.

Ripoti imeeleza kuwa robo tatu ya watoto hukosa maji na sabuni ya kunawa mikono majumbani mwao.
Ripoti imeeleza kuwa robo tatu ya watoto hukosa maji na sabuni ya kunawa mikono majumbani mwao.Picha: DW

Mkurugenzi mtendaji wa miradi katika UNICEF Sanjay Wijisekera amesema "Afrika inakabiliwa na janga la maji. Huku matatizo yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na yanayohusiana na maji yakiongezeka ulimwenguni, hakuna sehemu yoyote ulimwenguni ambayo hatari ya majanga hayo ni kubwa kwa watoto kama ilivyo barani Afrika".

Ameendelea kusema kuwa majanga kama vimbunga, mafuriko, na ukame wa kihistoria tayari yanaharibu mindombinu na majumba, yanachafua vyanzo vya maji, yanazidisha mgogoro wa njaa na kuenea magonjwa. Na kwamba endapo hatua za dharura hazitachukuliwa kudhibiti changamoto hizo basi mustakabali unaweza kuwa mbaya zaidi.

Tathmini hiyo ya kote ulimwenguni ilichambua huduma kwa jamii kulenga upatikanaji wa maji na mazingira safi, vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano kutokana na maji na mazingira machafu, na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ilibaini ni wapi haswa watoto wako katika hatari zaidi, na ni wapi uwekezaji unahitajika zaidi kuzuia vifo.

Upatikanaji wa maji safu ungali changamoto kwa nchi nyingi Afrika
Upatikanaji wa maji safu ungali changamoto kwa nchi nyingi AfrikaPicha: AP

Katika nchi 10 zilizotajwa, takriban theluthi moja ya watoto hawana angalau maji ya msingi nyumbani, na theluthi mbili hawana huduma za usafi. Robo ya watoto hawana chaguo ila kuenda haja katika viwanjani au vichakani. Wananawa mikono kwa nadra, kwani robo tatu ya watoto hawana maji na sabuni nyumbani.

Matokeo ya hayo yote ni kwamba mataifa hayo ndiyo hukabiliwa na vifo vingi vya watoto kutokana na maradhi kama kipindupindu yanayosababishwa na uchafu wa maji na mazingira

Kwa mfano sita kati ya nchi hizo10 zilikumbwa na mlipuko wa kipindupindu mwaka uliopita.

Wijisekera amehitimisha kwa kusema kifo cha mtoto ni pigo kubwa kwa familia, lakini huzuni huongezeka zaidi ikiwa kifo kimesababishwa na hali ambayo ingeepushwa kama ukosefu wa mahitaji ya msingi ikiwemo maji, vyoo na sabuni za kunawa mikono.

Vyanzo: UNICEF, DPAE