Umoja wa Mataifa waidhinisha upelekaji misaada Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa waidhinisha upelekaji misaada Syria

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha ruhusa kuingia kwa misaada ya kiutu katika maeneo ya waasi bila ya ridhaa ya serikali ya Syria katika maeneo manne ya vivuko mpakani na Uturuki, Iraq na Jordan.

UN Sicherheitsrat Resolution Syrien 22.5.2014

Baraza la Usalama likipiga kura kuhusu azimio kuhusu Syria

Hata hivyo Syria imetoa onyo kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa inaiangalia hatua hiyo ya kupeleka misaada kuwa ni kuingilia ndani ya mipaka yake.

"Ridhaa ya maafisa wa Syria haitakuwa muhimu tena," balozi wa Luxembourg katika Umoja wa Mataifa Sylvie Lucas amewaambia wajumbe 15 wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kura kuhusu azimio hilo, ambalo liliandaliwa na Luxembourg, Australia na Jordan.

Ramadan Armenspeisung Syrien Aleppo

Wakimbizi wa ndani wa Syria wakipatiwa msaada wakati wa mfungo wa ramadhan

Azimio hilo ambalo lilipitishwa kwa kauli moja litakalodumu kwa muda wa siku 180 na mfumo wa uchunguzi kwa ajili ya upakiaji wa shehena ya misaada katika milolongo ya magari katika nchi jirani, ambazo zitaiarifu tu Syria kuhusu aina ya msaada huo wa kiutu katika shehena hizo.

Watu milioni kadha wanahitaji msaada

Umoja wa mataifa umesema kuwa kiasi ya watu milioni 10.8 nchini Syria wanahitaji msaada, ambapo watu milioni 4.7 wako katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa.

Kiasi ya watu 150,000 wameuwawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria , ambavyo viko katika mwaka wa nne hivi sasa.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power ameishutumu serikali ya Syria kwa kutumia kuzuwia misaada , kama "silaha nyingine katika hazina ya silaha zake za maangamizi na za kikatili dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na upinzani."

Irak Armee Jurf al-Sakhar 30.06.2014

Majeshi ya serikali yakipambana na waasi nchini Syria

Serikali ya Syria imelionya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita kuwa kupeleka misaada kupitia katika mipaka kwenda katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi bila ridhaa itakuwa sawa na shambulio dhidi ya nchi hiyo.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Ja'afari ameliambia baraza hilo baada ya kura iliyopigwa jana kuwa serikali ya Syria inategemea jukumu lisilo elemea upande wowote, linalotekelezeka na la uwajibiukaji kutoka kwa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia hali ya kiutu nchini Syria, hususan inapokuja suala la kuheshimu mipaka ya Syria.

Syrischer UN-Botschafter Bashar Ja'afari Abkommen zu Chemiewaffen

Balozi wa Syria katika umoja wa mataifa Bashar Ja'afari

Azimio hilo pia linaidhinisha upelekaji wa misaada kuvuka mipaka ya maeneo yenye mzozo.

Bashar al-Assad kuapishwa Alhamis

Wakati huo huo rais Bashar al-Assad katika sherehe za kuapishwa siku ya Alhamis anatarajia kujiweka katika hali ya kuwa "mshindi " wakati akijaribu kuwavutia Wasyria ambao wamechoshwa na vita pamoja na wale ambao wanahofia kusonga mbele kwa makundi ya kijihadi.

Abu Bakr al-Baghdadi

Kiongozi wa kundi la Taifa la Kiislamu Abu Bakr al-Baghdadi

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Assad ambaye amerejeshwa madarakani katika uchaguzi wa hapo Juni 3 ambao umeshutumiwa kuwa ni kichekesho na upinzani, pia atajaribu kuyashawishi mataifa ya magharibi kuwa utawala wake ni ngome dhidi ya kundi la Waislamu wenye imani kali la Taifa la Kiislamu IS, ambalo linaendesha mapambano ya kigaidi nchini Syria na Iraq.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com