Umoja wa Afrika yasitisha uwanachama wa Burkina Faso | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Afrika yasitisha uwanachama wa Burkina Faso

Umoja wa Afrika umesitisha uwanachama wa Burkina Faso na kuwawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi wakati wanajeshi wakifyatuwa risasi kuwazuwiya waandamamaji kuandamana kwenye Uwanja wa Mapinduzi nchini humo.

Generali Gilbert Diendere kiongozi wa mapinduzi ya Burkina Faso.

Generali Gilbert Diendere kiongozi wa mapinduzi ya Burkina Faso.

Umoja wa Afrika umesitisha uwanachama wa Burkina Faso katika umoja huo na kuwawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi wakati wanajeshi wakifyatuwa risasi kuwazuwiya waandamamaji kuandamana kwenye Uwanja wa Mapinduzi nchini humo.

Umoja huo wa Afrika wenye nchi wanachama 53 umwewawekea marufuku ya safari na kuzuwiya mali za viongozi hao wa kijeshi huku mwakilishi wa Uganda akishutumu kutekwa nyara kwa viongozi wa Burkina Faso hapo Jumatano na kikosi maalum cha kijeshi kilicho tiifu kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Blaise Compaore kuwa "ni kitendo cha ugaidi."

Balozi wa Kenya katika umoja huo Mull Katende ameongeza kusema "hatua zote zilozochukuliwa na wale walionyakuwa madaraka kwa nguvu ni batili.

Ujumbe huo mkali wa Umoja wa Afrika unakuja wakati Rais Macky Sall wa Senegal mwenyekiti wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS na Rais wa Benin Thomas Boni Yayi wakiwasili mjini Ouagadougou katika juhudi za kuupatia ufumbuzi mzozo huo.

Tayari wamekutana kwa mazungumzo na kiongozi wa mapinduzi hayo Generali Gilbert Diendere mkuu wa zamani wa majeshi wakati wa utawala wa Compaore.

Waandamanaji wapinga mapinduzi

Kikosi maalum cha ulinzi wa rais kilichoonoza mapinduzu Burkina Faso..

Kikosi maalum cha ulinzi wa rais kilichoonoza mapinduzu Burkina Faso..

Wakati viongozi hao wakiwasili wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais ambacho ndicho kilichoongoza mapinduzi hayo walifyatuwa risasi hewani kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuandamana kuelekea Uwanja wa Mapinduzi mjini Ouagadougou ambao ulikuwa kitovu cha uasi wa umma uliomuondowa madarakani Compaore hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2014.

Alilazimika kuikimbia nchi hiyo baada ya kujaribu kuurefusha utawala wake wa miaka 27 wa taifa hilo la kimaskini Afrika magharibi.

Kikosi hicho maalum cha ulinzi wa rais cha Compaore RSP kimenyakuwa madaraka rasmi hapo Alhamisi baada ya kulalamika kwamba serikali ya mpito nchini humo inayoongozwa na rais wa muda Michel Kafando inawatenga wafuasi wa zamani wa rais kushiriki katika uchaguzi wa tarehe 11 mwezi wa Oktoba.

Viongozi wa mapinduzi wamemuachilia Kafando na mawaziri wawili hapo Ijumaa kwa kusema kwamba hiyo ni ishara ya kutuliza hali ya mvutano lakini waziri mkuu Isaac Zida afisa wa zamani katika kikosi hicho cha ulinzi wa rais cha RSP anaendelea kubakia katika kizuizi cha nyumbani.

Maandamano yazagaa

Mwandamanaji anayepinga mapinduzi Burkina Faso.

Mwandamanaji anayepinga mapinduzi Burkina Faso.

Maandamano ya kupinga mapinduzi yamezidi kuzagaa katika miji kadhaa.Katika mji mkuu wa kiuchumi nchini humo wa Bobo-Dioulasso wanawake walikuwa wamekusanyika wakiwa wamebeba miko mipana na mifagio ishara za kundi la vuguvugu la kiraia la Balai Cotoyen ikimaanisha "Fagio la Kiraia "ambalo mwaka jana lilikuwa mstari wa mbele katika maandamano dhidi ya Compaore wakionyesha kwamba wanataka kuzisafisha siasa za nchi hiyo.

Burkina Faso ilikuwa ikijiandaa kwa uchaguzi wake wa kwanza wa demokrasia kufanyika nchi humo baada ya miongo mingi kabla ya mapinduzi hayo kuitumbukiza demkrasia changa ya nchi hiyo kwenye machafuko.

Kiongozi wa mapinduzi hayo Generali Diendere amekanusha kwamba mapinduzi hayo yameandaliwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Compaore ambako mahali aliko hakujulikani.

Lakini wachambuzi wanatilia mashaka taarifa kwamba Compaore yumkini akawa haelewi chochote kuhusu mipango hiyo ya mapinduzi yaliofanywa na msaidizi wake wa zamani.

Compaore aliitawala nchi hiyo tokea aiingie madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1987 yaliopelekea kifo cha kutatanisha cha Rais Thomas Sankara ambaye kwa wengi bado anahesabiwa kuwa shujaa wa mapinduzi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Isaac Gamba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com