1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa ECOWAS kukutana na waliopindua serikali Guinea

Grace Kabogo
9 Septemba 2021

Ujumbe wa viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS unatarajiwa kuwasili Guinea Alhamisi kukutana na wanajeshi walioipindua serikali ya Rais Alpha Conde.

https://p.dw.com/p/4083f
Ghana Accra| ECOWAS zur Lage in Mali | Nana Akufo-Addo
Picha: Nipah Dennis/AFP/Getty Images

Viongozi hao wanatarajiwa pia kutathmini hali ilivyo nchini Guinea baada ya mapinduzi yaliyofanywa na kikosi maalum cha jeshi nchini humo.

Maafisa wa ngazi ya juu wa ECOWAS wanatarajia kukutana na maafisa wa kijeshi kwenye mji mkuu wa Guinea, Conakry na kuwashinikiza wairejeshe mara moja nchi hiyo kwenye utawala wa katiba.

Jumuia hiyo yenye nchi 15 wanachama imeisimamisha Guinea uwanachama kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya.

Viongozi wa ECOWAS waliokutana kwa njia ya mtandao, wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu mapinduzi hayo ya Septemba 5 na madhara yake kwa amani na utulivu wa kikanda.

Soma pia: Watawala wapya Guinea watafuta kujiimarisha madarakani

Jumuia hiyo imethibitisha kupinga kwake mabadiliko yoyote ya kisiasa yasiyofuata katiba na kulaani vikali mapinduzi hayo.

Mamady Doumbouya, kiongozi wa kikosi maalum kilichoipindua serikali ya Rais Alpha Conde akipungia mkono juu.
Mamady Doumbouya, kiongozi wa kikosi maalum kilichoipindua serikali ya Rais Alpha Conde akipungia mkono juu.Picha: CELLOU BINANI/AFP/ Getty Images

Ujumbe huo utaongozwa na Rais wa ECOWAS, Jean-Claude Kassi Brou na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Shirley Ayorkor Botchway. Hata hivyo jumuia hiyo haijatoa maelezo zaidi.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa ECOWAS amesema wamewataka viongozi wa mapinduzi kumteua waziri mkuu wa kiraia wa kuaminika haraka iwezakanavyo kwa lengo la kusaidia kuirejesha nchi hiyo katika kuheshimu katiba.

Soma pia: Ulimwengu walaani mapinduzi ya kijeshi Guinea

ECOWAS imewataka viongozi wa mapinduzi kuhakikisha usalama wa Rais Conde, pamoja na watu wote waliokamatwa kufuatia mapinduzi hayo. Conde bado anashikiliwa na wanajeshi hao, ambao wamesema kwamba yuko katika sehemu salama na anapata fursa ya huduma za matibabu. Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo amesema mapinduzi hayo ni ukiukaji wa hati ya kawaida ya kutawala katika jumuia ya ECOWAS.

''Jambo kuu ambalo limetuleta hapa, ambalo ni la kujutia, tukio la kusikitisha linaloendelea Guinea, ni kujadiliana kuhusu ukiukaji huu wa utawala bora ndani ya ECOWAS,'' amesema Akufo-Addo

Hata hivyo, uongozi huo wa kijeshi uliwaachia huru wanasiasa kadhaa wa upinzani waliokuwa wamefungwa wakati wa utawala wa Conde. Wote hao wamealikwa kuhudhuria mkutano wa kisiasa uliopangwa kufanyika siku ya Jumamosi mjini Conakry.

Guinea Alpha Conde
Picha: Facebook/Alpha Condé

Wengi wa walioachiwa huru ni wanaharakati wa chama kikuu cha upinzani nchini Guinea cha Union of Democratic Forces kinachoongozwa na Cellou Dalein Diallo, ambaye aligombea mara tatu katika uchaguzi wa urais na alishindwa na Conde.

Umoja wa Mataifa wayafuatilia matukio ya Guinea kwa karibu

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema unaendelea kuifuatilia kwa karibu hali inayoendelea Guinea. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema mratibu mwakilishi wa umoja huo nchini Guinea, Vincent Martin anaratibu juhudi za kutoa taarifa kwa washirika muhimu wa kimataifa.

Dujarric amesema timu ya Umoja wa Mataifa bado imejizatiti kuisaidia nchi hiyo, ikiwemo juhudi zinazoendelea za kukabiliana na athari kadhaa za janga la COVID-19, huku ikiufuatilia ugonjwa wa Ebola ambao ulitangazwa miezi mitatu iliyopita.

(APE, RTRE)