1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapinga kuondoa ulinzi wa hatimiliki za chanjo

Sylvia Mwehozi
7 Mei 2021

Ujerumani imepinga miito ya kuondoa ulinzi wa hatimiliki katika utengenezaji wa chanjo za Covid-19, ikisema uamuzi huo utakuwa na athari kubwa katika uzalishaji na kwamba hatimiliki zimekuwa chanzo cha ubunifu

https://p.dw.com/p/3t4re
Deutschland Corona-Pandemie Impfkampagne | Frankfurt am Main
Picha: picture alliance/dpa

Serikali ya Ujerumani imepinga wito uliotolewa na Marekani wa kuondoa ulinzi wa hatimiliki katika chanjo za virusi vya corona. Taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali inasema "mapendekezo ya Marekani kuondoa ulinzi wa hatimiliki za chanjo ya Covid-19 utakuwa na athari kubwa katika uzalishaji kwa ujumla".

Serikali badala yake, imesema uwezo wa uzalishaji na udhibiti wa ubora ndio nyenzo muhimu  katika upatikanaji wa chanjo na sio hatimiliki. Taarifa hiyo inasisitiza kwamba serikali ya Ujerumani inaunga mkono mpango wa kimataifa wa upatikanaji chanjo wa COVAX, unaolenga kuwapatia chanjo watu wengi ulimwenguni.

Kauli ya Ujerumani inakuja katika kujibu mabadiliko ya kisera ya Marekani ambapo Rais Joe Biden alitoa wito wa kuondolewa kwa muda ulinzi wa hatimiliki kama njia ya kuwezesha upatikanaji wa chanjo. Mwakilishi wa kibiashara wa Marekani Katherine Tai aliunga mkono majadilino hayo katika shirika la biashara duniani WTO.

Deutschland Symbolbild Impfzentrum Greifswald
Watu wakiwa katika foleni ya kupatiwa chanjoPicha: Stefan Sauer/dpa/picture alliance

Wito huo pia unaungwa mkono na Rais wa Halmashauri kuu ya umoja wa ulaya, Ursula von der Leyen ambaye amedai kwamba Brussels iko tayari kuyajadili mapendekezo hayo. Hatua hiyo pia ilipongezwa na Umoja wa Afrika, Ufaransa, Italia, Urusi na Austria pamoja na mkuu wa shirika la biashara ulimwenguni Ngozi Okonjo-Iweala. Rais wa afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepongeza wito huo akisema nchi yake ingependa kutengeneza chanjo yake yenyewe.

"Kama nchi, tunataka kutengeneza chanjo hapa ndani dhidi ya janga hili na majanga mengine. Ni kwasababu hii kwamba Afrika Kusini na India zilipendekeza kuondolewa ulinzi wa hatimiliki katika shirika la biashara duniai, ili kuwezesha uzalishaji wa chanjo za Covid-19 katika nchi zinazoendelea."

Wakati huo huo mkurugenzi mtendaji wa Pfizer, Albert Bourla amesema kampuni yake "haikubaliani kabisa" na hatua hiyo, akisisitiza kuwa hatimiliki sio kizuizi kikuu katika uzalishaji zaidi na kwamba ujenzi zaidi wa viwanda utakuwa ni hatua yenye manufaa.

Mataifa tajiri yamekabiliwa na tuhuma za kujikusanyia chanjo wakati nchi masikini zikihangaika kupata chanjo huku maambukizi ulimwenguni yakizidi kuongezeka. Wale wanaounga mkono mapendekezo hayo wanadai kuwa kupunguza vizuizi vya hatimiliki kutachochea utengenezaji wa chanjo kwa gharama nafuu na kuzisaidia nchi masikini ambazo zinajitahidi kuwapatia chanjo wananchi wake. India imekuwa ikiongoza mapambano hayo ya kuruhusu kampuni zaidi za dawa kutengeneza chanjo hizo, wakati ikikabiliwa na ongezeko la maambukizi na vifo kutokana na upungufu wa oksijeni.