Ujerumani yaduwazwa 3-1 na Slovakia | Michezo | DW | 30.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yaduwazwa 3-1 na Slovakia

Kichapo cha mabao matatu kwa moja dhidi ya Slovakia katika mchuano wa kirafiki kimempa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew kazi ya kufanya kabla ya kukichagua kikosi chake cha mwisho cha dimba la Euro 2016

Loew ana mkutano muhimu na madaktari wa timu ya taifa akihitaji hakikisho kuwa wachezaji muhimu wakiwemo nahodha Bastian Schweinsteiger na beki Mats Hummels watakuwa katika hali nzuri kabla ya kuanza dimba la kombe la mataifa ya Ulaya Juni 10 nchini Ufaransa.

Ana hadi usiku wa manane leo kukitaja kikosi chake cha wachezaji 23, baada ya kurejea katika kambi ya mazoezi ya timu ya Ujerumani nchini Uswisi, akiwa na mambo kadhaa ya kutafakari kutokana na kichapo cha 3-1 dhidi ya Slovakia mjini Augsburg hapo jana.

Joachim Löw

Kocha Loew anasema ameridhishwa na chipukizi kikosini

Loew aliwapa wachezaji kadhaa chipukizi nafasi ya kumwonyesha uwezo wao "Leo ilikuwa siku ya wachezaji wetu chipukizi, Leroy Sane, Bernd Leno ambao wamecheza kwa mara ya kwanza halafu katika kipindi cha pili, Julian Weigl, Julian Brandt, Joerg Kimmich. Kwa hiyo kulikuwa na shinikizo kubwa katika hali hiyo. Bila shaka huwa kunatokea kosa moja au jingine. Lakini wote wanne wameniacha na hisia nzuri mazoezini".

Loew sasa ana mchuano wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Hungary mjini Gelsenkirchen Jumamosi ili kuipiga msasa timu yake kabla ya Ujerumani kuelekea Ufaransa katika kambi yao ya Evian-les-Bains. Alipoulizwa nani atacheza mchuano dhidi ya Hungary, Loew alisema "tutatangaza hilo mara baaa ya kufikia maamuzi. Tutazungumza baada ya kila kitu kutulia, tuangalie mazoezi Jumatatu na tena Jumanne, na kisha tutaamua wachezaji watakaocheza. Tutangaza kwa wakati mzuri wakati tutafikia maamuzi".

Ujerumani – inayotafuta kombe la nne la Ulaya – itaanza kampeni yake ya Euro dhidi ya wapinzani katika Kundi C Ukraine mjini Lille Juni 12, kisha dhidi ya Poland mjini Saint-Denis Juni 16 na Ireland Kaskazini mjini Paris Juni 21.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef