1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Qatar zatiliana saini mkataba wa nishati

Josephat Charo
20 Mei 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekutana na emir wa Qatar Sheikh Tamim Bin Hamad al Thani mjini Berlin. Ujerumani na Qatar zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa karibu katika sekta ya nishati.

https://p.dw.com/p/4Be9u
Berlin | Pressekonferenz: Tamim bin Hamad Al Thani und Olaf Scholz
Picha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Kansela Scholzamesema Qatar itakuwa na jukumu kubwa muhimu katika mkakati wa Ujerumani kutaka kutanua vyanzo vyake vya gesi na kuondokana na gesi ya Urusi. Akizungumza leo na waandishi habari mjini Berlin, akiwa pamoja na Al Than, Scholz amesema Ujerumani itajenga miundombinu ili iwe katika nafasi ya kuagiza gesi kwa njia ya meli.

Sheikh al Thani ameelezea matumaini yake kwamba makubaliano yataafikiwa kati ya Marekani na Iran luhusu mpango wa nyuklia, na akaeleza utayari wake kufikia mwafaka. Kiongozi huyo wa Qatar pia amethibitisha kuwa Qatar ina mpango wa kuizuia Ujerumani gesi kuanzia mwaka 2024.

Hapo awali katika juhudi za kuondokana na utegemezi wa gesi ya Urusi serikali ya Ujerumani imekamilisha mkataba wa ushirikiano wa nishati na Qatar. Al Thani pamoja na waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck wa chama cha Kijani wamesaini mkataba wakati kiongozi huyo akiwa katika ziara ya kiserikali hapa Ujerumani. Wizara ya uchumi mjini Berlin imetangaza hivi leo kusainiwa kwa makubaliano hayo yanayonuiwa kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Mkataba huo wa nishati utainufaisha Ujerumani kupitia manunuzi ya gesi kutoka Qatar kutanua mahitaji yake ya gesi na wakati huo huo kuimarisha ushirikiano katika masuala ya gesi ya hydrojeni. Kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine, serikali ya Ujerumani inatafuta kwa haraka kujinasua na kuwa huru kutokana na uagizaji wa nishati kutoka Urusi na pia inategemea gesi kutoka Qatar, pamoja na vyanzo vingine.

Qatar yataka kuiletea Ujerumani gesi kuanzia 2024

Al Thani ameliambia gazeti la Uejrumani Handelsblatt kwamba wanataka kiwanda chao cha gesi cha Golden Pass kilichoko Texas nchini Marekani, kiwe tayari kusafiriha gesi hadi Ujerumani kuanzia wakati huo na mambo huenda yakafanyika haraka kuliko ilivyopangwa hapo awali.

Mbali na masuala ya nishati, mkataba huo utaimarisha mabadilishano ya taarifa kuhusu nishati, kujenga madaraja kati ya nchi hizo na kuwaleta pamoja wadau katika sekta ya umma na sekta binafsi. Mkataba huo pia unazungumzia kufanyika kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya wizara ya nishati ya Qatar na wizara ya uchumi na ulinzi wa mazingira ya serikali ya shirikisho ya Ujerumani.

Al Thani amesema Qatar ina matumaini ya kuukariisha ulimwengu kwa kombe la dunia la kandanda mwishoni mwa mwezi Novemba, lakini wanatarajia wageni waheshimu utamaduni wao.

Baadaye leo Sheikh al Thani anatarajiwa kukutana na rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier wakati wa zaira yake mjini Berlin.

Al Thani anazuru Ujerumani akitokea Uhispania na anatarajiwa pia kuitembelea Uingereza, Slovenia na Uswisi, ambako atahudhuria Jukwaa la kiuchumi la kimataifa huko Davos kati ya Mei 22 na 26.

dpa