1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kurekebisha masaibu yake dhidi ya Uholanzi

Sekione Kitojo
19 Novemba 2018

Timu ya taifa ya Ujerumani  Die Mannschaft, yataka kujiweka katika nafasi nzuri ya kupangwa katika makundi ya kombe la mataifa ya  Ulaya mwezi Desemba, itakapoingia uwanjani leo Jumatatu(19.11.2018) dhidi ya Uholanzi.

https://p.dw.com/p/38XVH
UEFA Nations League - Niederlande gegen Deutschland | Nationaltrainer Löw
Picha: picture-alliance/GES/M. Ibo Güngör

Kocha  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani Joachim Loew  amesema jana  Jumapili  kuwa  kiwango  cha  kukatisha  tamaa kilichooneshwa  na  timu  ya  taifa  katika  mwaka  2018 kinakatisha tamaa  na  sasa  kinalenga  katika  kile  mabingwa  hao  wa  zamani wa  kombe  la  dunia  wanahitajika  kufanya  ili  kurejea  katika  hali yake  ya  kawaida.

Fußball Länderspiel Russland - Deutschland Joachim Löw
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim LowPicha: Getty Images/AFP/R. Michael

Ujerumani  inakwaana  na  Uholanzi  leo Jumatatu  katika  mchezo  wao  wa  mwisho  wa  ligi  ya  mataifa , ambapo  tayari  wamekwisha  shuka  daraja, na  wanajaribu  tu kunusuru  mwaka  ambao  umekuwa  na  matatizo  makubwa  kwa kikosi  hicho kwa  kucheza  vizuri  leo  jioni.

Waliuanza  mwaka  huu wa  2018  wakiwa  mabingwa  watetezi  na  timu  iliyopigiwa  upatu kurejesha  kombe  la  dunia nyumbani  nchini  Urusi, lakini waliondoka  katika   michuano  hiyo  mapema  katika  muda  wa miaka  80  na  timu  hiyo  inaelekea  katika  mwaka  2019 ikiwa imefungwa  mara  sita hadi  sasa  katika  mwaka  mmoja. Mchezaji wa  ulinzi  wa  Die Mannschaft Joshua  Kimmich amesema kuporomoka  daraja  ni  lazima  tukuweke  mbali  na  tuanze  upya.

"Ndio, hali  ya  kushuka  kutoka  kundi  la  ligi  ya  mataifa, ni  lazima tusahau. Ni  wazi kwamba  kwetu kesho ni mchezo usio  na umuhimu, lakini tutauchukulia kwa  dhati  na  pia  tunataka  kushinda bila  kujali  ukweli  kwamba tuko wa mwisho  katika  kundi. Bila shaka  tunataka  kumaliza  mwaka  huu, ambao  ulikuwa  mbaya, kwa mchezo  mzuri."

Fußball  Löw beim Training Nationalmannschaft
Kikosi kipya cha Die Mannschaft Picha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Mwaka wa kukatisha  tamaa

Pigo la  mwisho  kwa  kikosi  cha  Joachim  Loew  lilikuja  siku  ya Ijumaa  wakati  kikosi  cha  Uholanzi  kilipoishinda  Ufaransa  na kuhakikisha  kwamba  Ujerumani  inashuka  daraja  katika mashindano  hayo  mapya  ya  ligi  ya  mataifa. Kocha  Joachim Loew  alikuwa  na  haya  ya  kusema.

"Inasikitisha  kwetu , bila  shaka, kwa  mchezo  wa  kesho,  kwamba hatuwezi  kubadili  chochote hivi  sasa  inapokuja  katika  ligi ya mataifa. Wiki  iliyopita, nilisema  kwamba  ninapaswa  kukubali kwamba  mwaka  huu  ulikuwa  wa kukatisha  tamaa  sana, kwamba tunajifunza mambo  muhimu  na  tunachukua hatua  sahihi kwa  ajili ya  mwaka  ujao na  mwaka  2019  na  hapo  baadae na  katika michuano  ya  mwaka  2020."

Lakini  kuna  matumaini  ya  hapo  baadaye kwa  kuijenga  upya  timu ya  taifa  ya  Ujerumani kutokana  na  vijana  chipukizi  kama  zilivyo timu  nyingine  za  taifa. Loew  alimwacha  mlinzi  wa  kati  Jerome Boateng katika  michezo  miwili  na  kuwaacha  katika  benchi wachezaji  wengine  wawili  wazoefu Thomas Mueller  na  Mats Hummels. Leo huenda kikosi  hicho  kikacheza  bila mchezaji  wa pembeni  Marco  Reus, ambaye  ana  maumivu  madogo  ambayo yamesababisha  pia  kutocheza  dhidi  ya  Urusi. Loew tena.

Joachim Löw Jerome Boateng
Jerome Boateng (kulia) na kocha wa taifa Joachim Low (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/I. Fassbender

"Ni kipi kingine kinaweza  kuwa  muhimu , ni mchezo hapo  kesho kwa ajili  ya  kuingia katika chungu sahihi cha  kupangwa katika  makundi kwasababu timu 10 za kwanza  katika  kundi A zinatoka  katika chungu cha  kwanza. Kwa  hiyo Iceland iko nyuma  yetu, Poland ina pointi moja, sisi  tuna pointi moja, kwa  hiyo  matokeo ni  muhimu kwetu  ili tuwe  katika  chunga  namba  moja  Desemba  2. Sababu nyingine  muhimu ni  kama  nilivyosema, tunataka  kuuaga  mwaka huu vizuri, kwa  mchezo mzuri. Kwetu sisi, na  bila  shaka  kwa mashabiki  wetu, pia  kuonesha  tuko  katika  njia  sahihi  ya kufufuka."

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / ape / afpe / rtre

Mhariri:  Yusuf , Saumu