Uchaguzi wa Thailand wafutiliwa mbali na mahakama ya kikatiba | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Thailand wafutiliwa mbali na mahakama ya kikatiba

Mahakama ya kikatiba ya Thailand imefutilia mbali uchaguzi mkuu uliofanywa nchini humo tarehe 2 mwezi uliopita kwa misingi ya kuwa upigaji kura haukufanywa kote nchini siku hiyo moja.

Majaji sita kati ya tisa wa mahakama hiyo ya katiba walipiga kura kufikia uamuzi huo wa kutupilia mbali uchaguzi huo ambao ulisusiwa na chama kikuu cha upinzani cha Thailand.

Msemaji wa mahakama Phimon Thampitakpong amesema uchaguzi huo haukuendeshwa katika siku moja kote nchini humo na hiyo ndiyo sababu ya kufutiliwa mbali.

Mahakama hiyo sasa imeiagiza tume ya uchaguzi kushauriana na serikali ya Waziri mkuu Yingluck Shinawatra ambaye alikuwa ameitisha uchaguzi huo wa mapema wa mwezi Februari ili kukubaliana kuhusu tarehe mpya ya kuandaliwa kwa uchaguzi mwingine.

Uchaguzi mpya kuandaliwa

Katika uchaguzi huo wa terehe 2 mwezi jana,upigaji kura haukufanyika katika maeneo 28 kati ya 375 ya uwakilishi bungeni maeneo hayo yote yakiwa katika majimbo yaliyoko kusini mwa Thailand ambako ni ngome za chama cha Democrat cha upinzani.

Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra

Waziri mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra

Chini ya katiba ya nchi hiyo uchaguzi mkuu unapaswa kufanyika katika maeneo yote siku moja.Kutokuwepo matokeo katika maeneo 28 ya uwakilishi kunamaanisha kuwa serikali mpya haingeweza kuundwa kwani sheria inataka angalau asilimia 95 ya viti vya bunge vijazwe ili kuitisha vikao vya bunge jipya

Waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali ya Yingluck walizuia usajili wa wagombea na shughuli za uchaguzi kufanyika katika maeneo hayo.

Chama tawala Pheu kilishiriki uchaguzi huo bila kupingwa baada ya upinzani kuususia kwani wanamtaka Yingluck kuondoka madarakani kwa shutuma za ufisadi na kuwa kibaraka wa kaka yake aliyeondolewa madarakani Thaksin Shinawatra.

Upinzani watishia kususia uchaguzi tena

Msemaji wa chama cha upinzani Chavanond Intarakomalayasut alionya hapo jana kuwa chama hicho huenda ikaususia uchaguzi ujao pia iwapo utafanyika kabla ya kupata hakikisho kuwa utaendeshwa kwa njia huru na ya haki na kuwepo kamati inayozishiriisha pande zote kutekeleza mageuzi ya kisiasa.

Waandamanaji katika mji mkuu Bangkok wakiupinga uchaguzi

Waandamanaji katika mji mkuu Bangkok wakiupinga uchaguzi

Kuambatana na katiba ya Thailand iwapo chama hicho cah Democrats kitasusia chaguzi mbili mfululizo kinakabiliwa na hatari ya kuvunjiliwa mbali kama chama cha kisiasa.

Uamuzi huo mahakama ni pigo jingine kisheria kwa waziri mkuu Yingluck ambaye anakabiliwa na shinikizo za kumtaka ajiuzulu na amesimama kidete kuwa hatang'atuka madarakani licha ya maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

Yingluck pia anakabiliwa na kesi kadhaa mahakamani ambazo zinatishia uongozi wake.

Msemaji wa chama chake ameutaja uamuzi huo wa mahakama kama jambo la kusikitisha na kuongeza kuwa kufutiliwa mbali kwa uchaguzi huo kutatoa mfano mbaya.

Mnamo siku ya Jumanne,Thailand ilitangaza kumaliazika kwa hali ya hatari ilyokuwa imewekwa kwa takriban miezi miwli mjini Bangkok na viungani mwake baada ya kuboreka kwa usalam tangu maandamano dhidi ya serikali kupunguza makali yake kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com