1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubingwa wa Liverpool wawatia nguvuni

Lilian Mtono
23 Julai 2020

Watu tisa wamekamatwa nje ya uwanja wa klabu ya Liverpool wa Anfield baada ya mashabiki 3,000 kupuuzia vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona na kukusanyika kushangilia ubingwa wa klabu yao.

https://p.dw.com/p/3fpaD
UK Liverpool-Fans feiern Meisterschaft
Picha: picture-alliance/Offside/A. Devlin

Baada ya klabu ya Liverpool kukabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi ya Premier ya England jana, watu tisa wamekamatwa nje ya uwanja wa klabu hiyo wa Anfield baada ya mashabiki 3,000 kupuuzia vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona na kuamua kukusanyika wakati wakisherehekea ubingwa wa klabu hiyo.

Kapteni wa klabu hiyo Jordan Henderson alikabidhiwa kombe hilo la ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 na mchezaji wa zamani na meneja Kenny Dalgish, katika uwanja huo ambao haukuwa na mashabiki baada ya kuwacharaza Chelsea kwa mabao 5-3.

Tangu kurejea viwanjani kwa ligi ya Premier mwezi Juni baada ya siku 100 za kusimamishwa, serikali ya Uingereza imezuia mashabiki kwenda kwenye viwanja vya michezo. Hii ni mara ya pili kwa mashabiki wa timu hiyo kupuuzia vizuizi hivyo. Kwa mara ya kwanza walikusanyika Juni 25 kusherehekea, baada ya Liverpool kuthibitishwa mabingwa wa ligi ya PL.

Polisi wa Merseyside bado wanawahoji watu 20 inaowashikilia tangu Juni 27. Miongoni mwao ni kijana wa miaka 19 aliekamatwa baada ya kuwasha moto kwenye jengo la kihistoria la Liverpool na watu 34 walijeruhiwa. Polisi hao wametoa agizo la watu wote kuwa wameondoka kwenye eneo la uwanja huo wa Anfield hadi kesho saa mbili na nusu usiku.

Mashirika: AFPE