1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubakaji wa wanawake bado ni tatizo Kivu Kaskazini

Benjamin Kasembe
24 Machi 2022

Kuongezeka kwa visa vya ubakaji dhidi ya wanawake kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini kunawatia wasiwasi watetezezi wa haki za binadamu pamoja na baadhi ya mashirika yanayotetea haki za wanawake.

https://p.dw.com/p/48yrD
Symbolbild Weltbevölkerungsbericht Frauen
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Idadi ya wanawake wanaoendelea kudhalilishwa kingono imeongezeka tofauti na miaka miwili iliyopita katika eneo hilo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. 

Gadhabu zimekuwa zikiongezeka katika baadhi ya mashirika ya kutetea haki za wanawake  mashariki mwa Kongo kutokana na kuongezeka kwa visa vya ubakaji na udhalilishaji wa kingono dhidi ya wanawake katika maeneo kadhaa ya Kivu Kaskazini haswa maeneo yanayokaliwa na makundi ya waasi.

Hata hivyo, kulingana na ripoti ya shirika la AIDPROFEN linalotetea haki za wanawake, ilikadiriwa kuwa zaidi ya wanawake 20 walibakwa na wengine wasiopungua 42 walinyanyaswa kingono kwenye kipindi cha mwezi mmoja uliopita. 

Masaibu ya wavuvi Ziwa Kivu

Sheria hapa nchini Kongo imeweka adhabu ya miaka 20 jela kwa kila kisa cha ubakaji dhidi ya wanawake, lakini mara nyingi bila kuzingatiwa zoezi linalokashifiwa na watetezi wa haki za binadamu kote hapa mashariki mwa Kongo ambao wanadai kuwa ni visa vichache vinavyochukuliwa hatua kisheria na kuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la visa hivyo, kama alivyoelezea CHRISTOPHE MUTAKA kutoka shirika linalotetea haki za wanawake la Martin Luther King.

Baadhi ya mashirika hayo ya kiraia yamedai pia kuwa usalama wa wanawake umeendelea kuwa mbaya zaidi tangu Rais Felix Tshisekedi alipotangaza amri ya kijeshi katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri ambamo hadi sasa operesheni za kijeshi bado zinaendelea. Kwa upande wake bunge la Kongo ambalo linafahamu pia kile kinachoendelea, hadi sasa limeahidi kuendelea kuwahimiza raia ili kupambana na tatizo la ubakaji na udhalilishaji wa kingono dhidi ya wanawake.

Kwa zaidi ya miongo miwili sasa, hali ya usalama wa raia imeendelea kuyumbishwa na makundi ya waasi yanayowatumia wanawake kama chombo muhimu cha kujikinga na vita.