Tyson Fury apokonywa taji la IBF | Michezo | DW | 09.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Tyson Fury apokonywa taji la IBF

Bondia Tyson Fury amepokonywa taji lake la ulimwengu la uzani mzito, IBF kwa sababu hatautetea mkanda huo dhidi ya mpinzani wa lazima. Hiyo imekuja ikiwa ni wiki mbili tu baada ya kushinda taji hilo

Muingereza huyo, ambaye ana mikanda ya WBO, WBA na IBO, badala yake anatarajiwa kupanda tena ulingoni kwa pigano la marudio na Wladmir Klitschko baada ya kuushangaza ulimwengu kwa kumzidi nguvu Mukraine huyo katika pigano la ubingwa wa dunia mwezi jana.

Shirikisho la kimataifa la ndondi IBF lilikuwa linataka apigana na mpinzani wake anayepigiwa upatu Vyacheslav Glazkov kabla ya kupigana na bondia yeyote yule.

Mwenyekiti wa shirikisho la ndondi la kimatafa IBF Lindsey Tucker, aliithibitishia BBC kuwa Fury amepokonywa ukanda huo wa uzani mzito akisema ''Kwa mujibu wa shirikisho letu Fury alipaswa kuzichapa dhidi ya mpinzani mkuu wa ukanda huu ambaye ni Vyacheslav Glazkov badala yake Fury mwenye umri wa miaka 27 aliamua kutimiza mkataba wa mechi ya marudio dhidi ya Klitschko''

Mkanda mwingine wa uzani wa juu WBC unashikiliwa na bondia kutoka Marekani Deontay Wilder.

Kimsingi Ukanda huo wa IBF unarejea Ukraine kwani Glazkov, mwenye umri wa miaka 31 ni raia wa Ukraine, na ameshinda mapigano 21 kati ya 22 aliyoshiriki.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com