1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuchel aizungumzia mipango yake na PSG

21 Mei 2018

Kocha mpya wa Paris St Germain – PSG Thomas Tuchel amesema kuwa ana furaha kuanza kuanza kufanya mazoezi na wachezaji wa klabu hiyo

https://p.dw.com/p/2y4Gh
Paris St. German Vorstellung Trainer Tuchel
Picha: Reuters/P. Wojazer

PSG walimgeukia kocha huyo Mjerumani hatimaye kuipiga jeki rekodi ya klabu hiyo katika ligi ya Mabingwa baada ya miaka kadhaa ya kutofanya vizuri. Tuchel mwenye umri wa miaka 44 aliyetokea Borussia Dortmund, anasema mafanikio hayatakuja haraka "vitu vidogo ndivyo huwa vitu vikubwa, hicho ndicho nnachoamini katika kila klabu. malengo huwa ya juu kabisa katika klabu hii, malengo yangu kawaida huwa ya juu sana kama nilivyosema awali. na bila shaka, tupo hapa kushinda, lakini pia ni mapema kuyazungumzia mambo mambo makubwa, ni muhimu sana kuwa tuanze kuyazungumzia mambo madogomadogo na sio tu kuzungumza bali pia kuyatekeleza".

Paris St. German Vorstellung Trainer Tuchel
Tuchel amesaini mktaba wa miaka miwiliPicha: picture-alliance/dpa/Maxppp/O. Arandel

Alisaini mkataba wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Mhispania Unai Emery ambaye alitwaa mataji matatu ya nyumbani msimu huu lakini akashindwa kuifikisha mbali PSG katika jukwaa kubwa la kandanda Ulaya.

Tuchel sasa ana fursa ya kuwapa mafunzo wachezaji nyota kama vile Neymar ambaye alisajiliwa na PSG kwa kitita kikubwa cha fedha "Neymar ni msanii, mchezaji mzuri sana, ni mmoja wa wachezaji bora duniani na wasanii huwa wachezaji  maalum na wanahitaji kulindwa kwa njia maalum ni kitu cha kawaida. tukipata njia ya kujenga timu kando yake, kujenga mfumo ambao anaweza kuutumia kuonyesha kipaji chake uwanjani, nadhani tuna mchezaji muhimu wa kutusaidia kushinda mechi zetu na niliupenda sana mkutano kati yangu na yeye. Nilikutana na kijana mnyenyekevu sana kwa mara ya kwanza".

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohamed Khelef