1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za Bundesliga zaunga mkono vuguvugu la kupinga ubaguzi

Deo Kaji Makomba
8 Juni 2020

Timu mbalimbali katika Bundesliga, zilipiga magoti kama ishara ya kuunga mkono harakati za maisha ya watu weusi ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/3dT3g
Deutschland Bundesliga - Werder Bremen v VfL Wolfsburg
Picha: Imago Images/gumzmedia/nordphoto/V. Witters

Wiki moja mara baada ya wachezaji Weston McKennie, Jadon Sancho na wengineo kutoa taarifa zao binafsi kuunga mkono harakati za maisha ya watu weusi, klabu zinazoshiriki ligi ya Bundesliga zimeonyesha mshikamano wao wa pamoja kupinga vikali vitendo vya ubaguzi wa rangi.

Wakati maandamano makubwa dhidi ya ukatili wa polisi na mfumo wa kibaguzi yaliendelea kufanyika duniani kote mwishoni mwa wiki iliyopita. Timu za Bundesliga zilionyesha uimara wao wa kuunga mkono kwa harakati hizo za watu weusi kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi.

Jumamosi (06.07.2020) wachezaji wa klabu ya Bayern Munich wakati wakipasha misuli moto kabla ya kuanza kwa mchezo wao wa ligi, walivalia tisheti zilizokuwa na ujumbe wa wazi. Wakati wa mchezo huo walionyesha kukerwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi huku wakionyesha kuunga mkono harakati za maisha ya watu weusi za kupinga vitendo hivyo vya ubaguzi wa rangi.

Kocha wa Bayern Munich, Hansi Flick, alisema wazo lilikuwa linatokana na timu hiyo kabla ya kuongeza kuwa ubaguzi wa rangi haupaswi kuwa suala tena lakini kwa bahati mbaya ni kwa sababu bado kuna watu wengi ambao wanaguswa tofauti.

Siku moja badaye, wachezaji wa klabu ya Borussia Dortmund wakati wakifanya mazoezi kabla ya mchezo wao wa ligi kuu ya Bundesliga, pia walivalia tisheti zilizokuwa na ujumbe wa wazi kupinga kuhusu ubaguzi wa rangi.

Borussia Dortmund - Hertha BSC Berlin I Protest gegen Rassismus
Jadon Sancho, akiwa na fulana yenye ujumbe "Bila Haki, Hakuna Amani"Picha: picture-alliance/T. Groothuis

Jadon Sancho ambaye awali wiki iliyopita alionyesha kuunga mkono kupinga vitendo hivyo vya kibaguzi baada ya kuonyesha ujumbe katika tisheti aliyokuwa ameivaa ukidai haki kwa George Floyd huku mchezaji mwenzake Achraf Hakimi alivalia tisheti yenye ujumbe uliosema kuwa bila haki hakuna amani. Nazo tisheti za viuongo, Axel Witsel na Emre Can, zilionyesha maneno yasemayo, "mweusi”, "mweupe” na "njano” walijumuika nje na neno "ubinadamu”.

Kabla ya mchezo wao dhidi ya Hertha Berlin kuanza wachezaji wote walipiga magoti katikati mwa uwanja wakiungana na mwamuzi wa mchezo huo, Tobias Stieler, na msaidizi wake. Pembeni mwa msitari wa uwanja watu wa benchi la ufundi nao walipiga magoti.

Naye kiuongo wa klabu ya Mainz, Pierre Kunde, pia alipiga magoti baada kufunga bao lake wakati wakicheza mechi ya Bundesliga dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Bundesliga - Borussia Dortmund v Hertha BSC
Wachezjai wa Borussia Dortmund na Hertha Berlin wakipiga magoti kabla mechi yao Juni 6, 2020Picha: Reuters/L. Baron

Maandamano hayo yalikuwa pia katika mechi za ligi ya daraja la tatu wakati Waldhof Mannheim na Viktoria Cologne pamoja na wasimamizi wa mechi walipiga magoti wakati spika za matangazo ya umma uwanjani hapo zilikuwa zikitangaza ujumbe wa kupinga ubaguzi wa rangi kabla ya mechi hiyo.

Siku iliyofutia, Werder Bremen na Wolfsburg pia walipiga magoti kuonyesha ishara ya kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi kama pia walivyofanya Union Berlin na Schalke.

Wiki iliyopita shirikisho la soka nchini Ujerumani, DFB, liliamua kwamba halitawaadhibu wachezaji kutokana na kuonyesha kwao kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi, likisema wachezaji wako huru kuonyesha hisia zao kwa kuunga mkono maandamano ya kupinga mauaji ya George Floyd. Taarifa ya DFB ilikuja kufuatia masuala ya kisiasa yakiwa yamepigwa marufuku wakati wa michezo kulingana na sheria za shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA.

Deo Kaji Makomba