Mbeki awasilisha hati za kujiuzulu.
22 Septemba 2008JOHANENNESBURG.
Chama kinachotawala nchini Afrika Kusini ANC, leo kinatarajia ,kumteua kaimu-kiongozi baada ya rais Thabo Mbeki kuwasilisha hati za kujiuzulu.
Chama hicho kilichukua hatua ya kumtoa bwana Mbeki madarakani ili kuutatua mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao haujawahi kukikabili chama cha ANC tokea kumalizika mfumo wa kibaguzi nchini Afrika Kusini.
Chama cha ANC kimemtoa Mbeki madarakani kabla ya muda wake rasmi wa urais kumalizika hapo mwakani. Hatua hiyo ilichukuliwa siku nane baada ya hakimu kutupilia mbali mashtaka ya rushwa dhidi ya kiongozi wa chama hicho bwana Jacob Zuma.
Katika uongozi wake Mbeki alifanikiwa kudumisha kipindi kirefu cha ustawi wa uchumi na alitoa mchango mkubwa katika utatuzi wa migogoro kusini mwa Afrika.
Mbeki amesema anaheshimu uamuzi wa chama chake na kwamba ataendelea kuwa mwanachama mtiifu.
Habari zinasema spika wa bunge Baleka Mbete anatazamiwa kuteuliwa kuwa kaimu rais.