1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaNepal

Tetemeko la ardhi nchini Nepal lauwa watu 138

Angela Mdungu
4 Novemba 2023

Idadi ya waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotikisa magharibi mwa Nepal Ijumaa usiku imefikia watu 138.

https://p.dw.com/p/4YOlN
Erdbeben in Nepal
Tetemeko la ardhi lililotokea Nepal na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100Picha: picture alliance/dpa/ZUMA Press Wire

Takwimu hizo zimetolewa leo na wizara ya mambo ya ndani ya Nepal wakati vikosi vya usalama vikifanya hima kusaidia katika juhudi za uokoaji.  Naye msemaji wa polisi katika mji mkuu Kasmandu amesema kuwa idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka. Takwimu za majeruhi na vifo katika baadhi ya maeneo yaliyopatwa na tetemeko hilo bado hazijapatikana. 

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Narayan Prasad Bhattarai alisema miongoni mwa waliokufa, 92 ni wa wilaya ya Jajarkot na 40 ni kutoka Rukum. Maeneo hayo mawili ndiyo yaliyoathiriwa vibaya zaidi na tetemeko hilo.

Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal  ametembelea eneo la mkasa, baada ya kuelezea kusikitishwa kwake na vifo, na uharibifu uliosababishwa na janga hilo.

Nepal imekuwa ikikumbwa mara kwa mara na matetemeko ya ardhi. Mwaka 2015, karibu watu 9,000 walikufa na wengine 22,000 walijeruhiwa baada ya tetemeko kubwa kuipiga nchi hiyo. Tetemeko hilo liliharibu takribani shule 8,000 na kuwaacha watoto wasiopungua milioni moja bila madarasa.