Tchad yatuhumiwea kutowalöinda ipasavyo raia | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Tchad yatuhumiwea kutowalöinda ipasavyo raia

Shirika la haki za binaadam latoa mwito tume ya umoja wa mataifa ipelekwe haraka Tchad

Wakimbizi wa Tchad

Wakimbizi wa Tchad

Katika ripoti yake iliyochapishwa mapema wiki hii,shirika linalopigania haki za binaadam Human Riths Watch linasema baraza la usalama linabidi liidhinishe haraka mpango wa kutumwa vikosi vya kimataifa mashariki ya Tchad ambako mashambulio yanaendelea dhidi ya raia wa kawaida.

Wiki ijayo, ofisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia opereshini za kulinda amani (DPKO) inatarajiwa kuliarifu baraza la usalama la umoja wa mataifa,juu ya mapendekezo ya Umoja wa mataifa kuhusu Tchad-kabla ya taasisi hiyo muhimu kuzingatia mpango halisi wa kutumwa wanajeshi katika eneo hilo.

Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita mashambulio dhidi ya raia wa kawaida yamekua yakipamba moto katika eneo la mashariki ya Tchad,karibu na mpaka wa Tchad na Sudan.Zaidi ya raia laki moja na 20 elfu wameyapa kisogo maskani yao kutokana na mashambulio dhidi ya vijiji vyao mashariki ya Tchad-wengi wao katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

“Tume ya Umoja wa mataifa inaweza kusaidia kuzuwia mashambulio dhidi ya raia nchini Tchad,ikiwa tuu itapatiwa nafasi ya kuendeleza shughuli zake ipasavyo” amesema mkurugenzi wa Human Rights Watch –tawi la Afrika Peter TAKIRAMBUDDE.”Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linabidi liipatie tume yoyote itakayopelekwa Tchad vifaa vyote vinavyohitajika,uungaji mkono wa kisiasa na ruhusa ya kutumia nguvu ikilazimika ili kuwalinda raia.”

Tchad inagubikwa na aina tatu za matumizi ya nguvu ambayo baadhi ya wakati, yanapishana moja baada ya jengine,yakizidisha makali ya mzozo wan chi hiyo na kuhatarisha maisha ya raia wasiokua na ulinzi wa aina yoyote.Kuna mashambulio yanyotokana na ugonvi wa ndani kati ya vikosi vya serikali na makundi ya wanaharakati wa upande wa upinzani ;kuna mashambulio ya mpakani yanayofanywa na wanamgambo wa Darfour dhidi ya raia wa kawaida wa Tchad na pia matumizi ya nguvu ya kimkoa.

Katika eneo la kaskazini mashariki GUÉRÉDA yalikotiwa saini makubaliano ya amani December mwaka jana kati ya serikali ya Tchad na kundi la waasi wa Tchad,hujuma za kikabila dhidi ya raia wa kawaida,naiwe zinazofanywa na waasi au wanamgambo,zimekua zikiendelea bila ya makundi hayo kuhofiwa chochote kile.

February 20 iliyopita kijiji cha Tama,umbali wa kilomita 15 kusini mwa mji wa Guéréda kiliripoitwa kutiwa moto na wanamgambo wa Zaghawa.Maafisa wa eneo hilo wamesema mashambulio hayo ni sehemu ya mfululizo wa mashambulio ya wanamgambo wa pande zote mbili dhidi ya raia wanaotuhumiwa kuelemea upande huu au ule.

Licha ya hujuma hizo,serikali ya Tchad imejizatiti kupambana pekee na kitisho kinachotokana na waasi wa tchad walioko Darfour.Kwa namna hiyo wamehamishiuwa kwengine na kuwaacha raia wakikabiliwa na kitisho cha kuweza kushambuliwa na wanamgambo wa Tchad kwenyewe ,pamoja pia na mashambulio ya mpakani toka Sudan.

Mbali na kushindwa kuwalinda raia,serikali ya Tchad inapalilia pia mivutano ya kikabila kwa kuwapatia silaha baadhi ya raia-ikiwa kama sehemu ya mkakati wa kupambana na waasi.

“Serikali ya Tchad haiwahifadhi raia wake.Kimsingi inawasukuma katika balaa kubwa zaidi kwa kukosekana usalama katika eneo la mpakani” amesema TAKIRAMBUDDE aliyesisitiza haja ya kutumwa wanajeshi wa kimataifa kuwalinda raia hayo.

Tume ya Umoja wa mataifa inayotazamiwa kupelekwa Tchad itabidi iwe na nguvu za kutosha kuweza kuzuwia hujuma dhidi ya raia,kulinda njia inakopitia misaada ya kiutu,kupiga doria katika mpaka wa Tchad na Sudan na kuchunguza nyendo za makundi ya wanamgambo na silaha zao.Zaidi ya hayo panahitajika kundi la watetezi wa haki za binaadam na kikosi cha polisi watakaokua na jukumu la kusaidia kuunda taasisi za kisheria na polisi na kusaidia kuwafikisha mahakamani wale wote waliovunja haki za binaadam.

Shirika la Human Rights Watch-tawi la Afrika limelisihi baraza la usalama liidhinishe haraka mapendekezo ya ofisi ya Umoja wa mataifa inayosimamia shughuli za kulinda amani-DPKO pamoja na kupitisha azimio linaloruhusu kutumwa wanajeshi wa Umoja wa mataifa nchini Tchad.

 • Tarehe 22.02.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJV
 • Tarehe 22.02.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJV

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com