1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania inaomboleza kifo cha rais wake John Magufuli

Amina Mjahid
18 Machi 2021

Tanzania inaomboleza kifo cha rais wake John Pombe Magufuli kufuatia wiki kadhaa za masuali yaliokosa majibu juu ya afya yake. Magufuli amefariki dunia wakati kukiwa na hisia mseto juu sifa za uongozi wake.

https://p.dw.com/p/3qnmd
Tansania Präsident John Magufuli verstorben
Picha: AFP

Bendera knchini Tanzania zinapepa nusu mlingoti na taifa limeingia katika kipindi cha maombolezo cha siku 14 baada ya makamu wa rais Samia Suluhu Hassan anaetarajiwa kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo kutangaza kifo cha Rais John Magufuli jana usiku.

Samia Hassan alisema Magufuli amefariki kutokana na matatizo ya moyo. Tangazo hilo limekuja baada ya serikali kukanusha kuwa rais anaumwa huku serikali hiyo ikiendelea kuwekewa shinikizo kuelezea wapi alipo kiongozi wa taifa, baada ya kukosa kuonekana hadharani kwa takriban wiki tatu, hali iliyosababisha wasiwasi na uvumi kwamba alikuwa nje ya nchi akipokea matibabu baada ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID 19. 

Lakini tarehe 17 mwezi Machi Makamu wa Rais Samia suluhu Hassan, akatangaza rasmi kifo cha kiongozi huyo aliyepewa jina la "tingatinga kwa jinsi alivyojipambanua kama mpambanaji dhidi ya ubadhirifu kwenye sekta ya umma.

soma zaidi: Upinzani Tanzania wataka Samia aapishwe mara moja kuwa rais

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye pia ni mwenyekiti Jumuiya ya Afrika Mashariki amejiunga na viongozi wengine kutoa salamu za rambirambi kwa taifa la Tanzania.

Kenyatta amesema Afrika kwa ujumla imempoteza kiongozi adhimu huku akiamuru Kenya kuingia katika kipindi cha maombolezo cha siku 7 na bendera kupepea nusu mlingoti katika eneo zima la Afrika Mashariki. Mataifa ya Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uingereza na Marekani pia yalituma salamu zao za pole huku Marekani ikisema inatumai Tanzania itasonga mbele kwa njia ya kidemokrasia.

Hisia mseto kuhus uongozi wa magufuli

Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania John MagufuliPicha: Tanzania Presidential Press Service

Hayati rais John Joseph Pombe Magufuli alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2015 kama mpambanaji dhidi ya rushwa na kuumpa sifa ya mtu asiyetaka mchezo na aliye na misimamo mikali.

Hatua yake ya kuitanua zaidi elimu ya bure usambazaji wa umeme katika sehemu za vijijini na uwekezaji wa katika miundo mbinu pia ilimfanya awe kipenzi cha wengi pamoja na juhudi zake za kuimarisha sekta ya madini na kudai mamilioni ya fedha kama ushuru kutoka kwa kampuni za madini

Lakini pia Magufuli alikosolewa kwa kuongoza kidikteta, akikandamizwa kwa vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na upinzani hali iliyopingwa vikali na washirika wake wa kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadaamu.

soma zaidi: Maoni: Magufuli, rais aliyependwa kama alivyochukiwa

Kuchaguliwa kwake tena kama kiongozi wa nchi katika uchaguzi wa Oktoba, kulipuuziliwa mbali na upinzani huku baadhi ya wanadiplomasia wakiutilia mashaka uchaguzi huo kufuatia ripoti za madai ya udanganyifu na vyombo vya habari vya kimataifa kunyimwa nafasi ya kuufuatilia wakiwa pamoja na makundi ya waangalizi wa kura.

Hayati Magufuli ni miongoni mwa viongozi wachache duniani, akiwa pamoja na rais wa Zamani wa Marekani Donald Trump na  rais  Jair Bolsonaro wa Brazil waliopouuza makali ya virusi vya corona na badala yake kugeukia tiba mbadala.

Aliitisha maombi kuliko kutoa tahadhari kwa watanzania kuvalia barakoa, kabla ya kusimamisha tangazo la takwimu zitokanazo na vifo na maambukizi ya virusi hivyo nchini mwake mnamo Aprili mwaka 2020. Wakati huo tanzania ilirekodi vifo 16 na idadi ya walioambukizwa walifikia 509.