Sudan kusini itakabiliwa na njaa hivi karibuni | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Sudan kusini itakabiliwa na njaa hivi karibuni

Shirika la Msaada la Uingereza, Disasters Emergency Committee limeonya kuwa Sudan Kusini itakabiliwa na janga la njaa mnamo wiki chache zijazo, ikiwa hakutakuwa na mpango kutoa kiasi kikubwa cha fedha kununulia chakula.

Südsudan Flüchtlingslager in Bor

Wakimbizi wa Sudan kusini nchini Ethiopia

Na kutokana na kitisho hicho cha njaa, maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanamiminika nchini Ethiopia kuepuka vita na ukosefu wa chakula. Zaidi ni katika taarifa ifuatayo iliyoandaliwa na Daniel Gakuba.

Katika tangazo la Disasters Emergency Committee, au DEC kwa kifupi, ambayo inajumuisha mashirika makubwa 13 ya msaada, imeelezwa kuwa ikiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vitaendelea, na wito wa fedha zaidi za msaada ukapuuzwa, maeneo kadhaa ya taifa hilo changa zaidi duniani yatakabiliwa na janga la nja ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

Sudanesische Flüchtlinge in Äthopien

Hali ya ukosefu wa chakula ni mbaya nchini Sudan kusini

Maelfu wamekwisha uwawa

Maelfu ya watu wamekwishauawa katika vita hivyo vilivyoanza Desemba mwaka jana, huku zaidi ya milioni 1.5 wakiwa wamelazimika kuyahama makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi UNHCR limesema kiasi cha fedha lilichonacho ni sawa na asilimia 40 ya mahitaji yake kununulia chakula cha kutosha kwa wakimbizi. Nakisi iliyopo katika bajeti ya shirika hilo ni ya takribani dola bilioni moja.

Mkuu wa DEC Saleh Saeedamesema kuna kitisho kilicho dhahiri katika maeneo mengi, kinachoashiria kwamba mamilioni ya watu wataathiriwa pakubwa na upungufu huo wa chakula.

Kulingana na viwango vya Umoja wa Mataifa, hali ya ukosefu wa chakula hugeuka janga pale asilimia 20 ya wakazi wa eneo fulani wanapokuwa wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kiwango cha utapiamlo kikiwaathiri asilimia 30 ya wakazi, na ikiwa kutakuwa na vifo vya watu wawili kila siku, katika eneo la wakazi elfu 10.

Ingawa mvua za msimu huu wa kilimo zinatarajiwa kuwa za kawaida au pungufu kidogo ya kiwango cha kawaida, Umoja wa Mataifa umesema sababu ya ukosefu wa chakula haina uhusiano na matatizo ya hali ya hewa, bali na mapigano baina ya serikali na waasi.

Südsudans Präsident Salva Kiir Mayardit

Rais Salva Kiir wa Sudan kusini

Fedha hazitoshi kwa sasa

Mashirika yaliyo ndani ya DEC ambayo ni pamoja na Oxfam, Tearfund na Save the Children, yana kiasi cha fedha ambacho hakifiki hata nusu ya mahitaji yake kuweza kuzuia Sudan Kusini isikabiliwe na baa la njaa.

Uhasama baina ya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar umesababisha kuenea kwa matatizo makubwa katika jamii.

Shirika la Umoja wa Mataifa WFP kwa ajilia ya Msaada wa Chakula limesema kwamba idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini inaendelea kumiminika nchini Ethiopia wakikimbia matatizo nchini mwao. Abdou Dieng ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo amesema kuwa tayari wakimbizi 158, 000 kutoka Sudan Kusini wamekwishawasili nchini Ethiopia tayari.

Südsudan Kämpfe 25.12.2013

Wanajeshi wa Sudan kusini wanapambana na waasi nchini humo

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba kila wiki Ethiopia hupokea wakimbizi zaidi ya 1,500. Umoja huo umeonya kwamba ikiwa hali hii itaendelea, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu Ethiopia itakuwa ikiwapa hifadhi wakimbizi zaidi ya laki tatu kutoka Sudan Kusini.

Na hali haiboreka nchini Sudan Kusini, kutokana na vita vinavyoendelea. Rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar walitia saini makubaliano ya tatu ya kusitisha uhasama, na kukubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika muda wa siku sitini, lakini bado vita vinaendelea licha ya makubaliano hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com