Steinmeier ataka serikali ya umoja wa kitaifa Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Steinmeier ataka serikali ya umoja wa kitaifa Afghanistan

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ametowa wito wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan kufuatia ziara yake ya ghafla nchini humo Jumamosi (06.09.2014).

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan(kulia) mjini Kabul.(06.09.2014).

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan(kulia) mjini Kabul.(06.09.2014).

Akiwa mjini Kabul Steinmeier amekutana na rais aliyoko madarakani Hamid Karzai na wagombea wawili wa uchaguzi wa rais uliozusha utata ambapo amewataka kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa mzozo huo wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa duru zilio karibu na ujumbe ulioandamana na Steinmeier katika ziara hiyo waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amewataka wagombea hao Abdullah Abdullah na Ashraf Ghani ambao amekutana nao katika nyakati tafauti kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa haraka kutokana na kwamba hakuna tena wakati wa kupoteza.

Ametowa wito wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayokuwa na uwezo wa kuchukuwa hatua na kufanya maamuzi kwa haraka.

Kinachohitajika ni nia

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan Hamid Sidiq katikati ni balozi wa Ujerumani nchini humo Markus Potzel mjini Kabul. (06.09.2014).

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan Hamid Sidiq katikati ni balozi wa Ujerumani nchini humo Markus Potzel mjini Kabul. (06.09.2014).

Steinmeier amekuwa muangalifu kwa matamshi yake ambapo amesema bado kuna vizingiti vingi, lakini sio kwamba visioweza kuepukwa, kile kinachohitajika ni nia ya kufikia muafaka kutoka pande zote mbili.

Amesema Afghanistan haipaswi kutumbukia tena kwenye mzozo kati ya makundi ya kisiasa au ya kikabila na kwamba ni muhimu maamuzi yakapitishwa kwa haraka ili kuwezesha shughuli za Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuendelea kwa kutowa mafunzo na ushauri kwa jeshi la Aghanistan baada ya muda wake kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Imeripotiwa kwamba Abdullah na Ghani walimwambia Steinmeier mazungumzo baina ya pande hizo mbili juu ya uwezekano wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yamepiga hatua fulani lakini kuna masuali mengi magumu ya kisiasa yalioendelea kukosa majibu ikiwa ni pamoja na mpango wa usalama utakvyokuwa kwa wanajeshi wa kigeni watakaobakia nchini humo baada ya kuondolewa kwa vikosi vya mapigano vya kimataifa.

Kiini cha mzozo

Wagombea hao wote wawili wanadai kuwa wameshinda uchaguzi wa rais wa Juni 14 na kusababisha mkwamo wa kisiasa uliozusha mvutano wa kikabila wakati vikosi vya mapigano vya NATO vikiongozwa na Marekani vikitarajiwa kuondolewa baada ya kuwepo nchini Afghanistan kwa miaka 13 kupambana na waasi wa kundi la Taliban.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na mgombea wa urais Abdullah Abdullah mjini Kabul.(06.09.2014)

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) akisalimiana na mgombea wa urais Abdullah Abdullah mjini Kabul.(06.09.2014)

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amewataka wanasiasa wa Afgganistan kutumia fursa ya kihistoria kukabidhiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia na ameahidi msaada wa Ujerumani katika kuunda serikali mpya ili mradi pande zote mbili zinakuwa tayari kushiriki.

Katika ziara yake hii Steinmeir pia alikuwa amepangiwa kukutana na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan Jan Kubis na waangalizi wa uchaguzi wa Ujerumani ambao amesema alikuwa na hamu ya kukutana nao.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo wagombea wote wawili wamedai kuwepo kwa udanganyifu wa kura na kwa kupitia upatanishi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pande hizo zilikubaliana kuhesabiwa upya kwa zaidi ya kura milioni nane chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ambapo hapo Ijumaa umetangaza kumalizika kuhesabiwa kwa kura hizo ambapo matokeo yake rasmi yanatarajiwa kutangazwa Jumatano.

Steinmeier aliwasili asubuhi katika kambi ya kijeshi ya Ujerumani ya Mazar -i- Shariff katika ziara yake hiyo iliowekwa siri kutokana na sababu za kiusalama.Baadae waziri huyo wa Ujerumani anaelekea India kukutana na serikali mpya ya Waziri Mkuu Narendra Modi.

Mwandishi : Mohamed Dahman / AFP/dpa/Reuters

Mhariri : Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com