Steinmeier afanya ziara ya ghafla Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Steinmeier afanya ziara ya ghafla Afghanistan

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amefanya ziara ya ghafla Afghanistan Jumapili(09.02.2014) na kuahidi kuendelea kuisaidia nchi hiyo baada ya kuondolewa kwa vikosi vya kigeni baadae mwaka huu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Rais Hamid Karzai mjini Kabul. (09.02.2014).

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Rais Hamid Karzai mjini Kabul. (09.02.2014).

Mwanasiasa huyo wa chama cha SPD amewasili katika makao makuu ya operesheni ya majeshi ya muungano kaskazini mwa Afghanistan katika mji wa Mazar- i- Sharif Jumapili asubuhi katika ziara yake ya kwanza tokea achaguliwe tena katika wadhifa huo wa waziri wa mambo ya nje baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akizungumza na wanajeshi 3,100 wa Ujerumani amesema "Hatukufanikisha kila kitu tulichokuwa tukitarajia " .Hata hivyo amesema kile walichofanikisha hakipaswi kudharauliwa na kwamba Ujerumani "inawajibika kusaidia kusalimisha kile kilichofanikiwa hadi sasa."Amesema huu sio mwaka muhimu kwa Afghanistan tu bali pia ni muhimu kwa maamuzi ya Ujerumani katika shughuli zake nchini humo.

Mazar-i-Sharif ni kambi ya mwisho yenye vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistan wakati vikosi vya kimataifa vikitazamiwa kufunga virago na kuhitimisha operesheni zake za mapigano mwishoni mwa mwaka huu nchini humo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Meja Generali Jörg Vollmer kamanda wa kikosi cha ISAF kaskazini mwa Afghanistan. (09.02.2014).

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Meja Generali Jörg Vollmer kamanda wa kikosi cha ISAF kaskazini mwa Afghanistan. (09.02.2014).

Baadae Steinmeier alikwenda katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul kukutana na Rais Hamid Karzai katika mazungumzo yaliyolenga miongoni mwa mambo mengine mustakbali wa Afghanistan baada ya kuondolewa kwa vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Karzai amegoma kusaini makubaliano ya usalama na Marekani kuhusu mipango ya kuendelea kuwabakisha kati ya wanajeshi 8,000 hadi 12,000 wa kimataifa nchini humo kutowa mafunzo kwa polisi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Licha ya Karzai kupata ridhaa ya kusaini makubaliano hayo kutoka kwa vionngozi wengine wa Afghanistan amesema kwamba mtu atakayerithi nafasi yake ndie anayepaswa kusaini makubaliano hayo.Kutokana na hatua hiyo ya Karzai serikali ya Marekani imetishia kuondowa vikosi vyake vyote vyenginevyo Karzai anasaini makubaliano hayo kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Aprili.

Suala hilo la uchaguzi pia limezunngumziwa katika mazungumzo kati ya Steinmeier na Rais Karzai ambaye ameiongoza nchi yake tokea mwaka 2011 baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Taliban na hawezi kugombania tena urais baada ya mihula miwili.

Wakufunzi na washauri

Pia wamezungumzia majukumu ya usoni ya kikosi cha Ujerumani "Bundeswehr" katika jimbo la Hindu Kush nchini Afghanistan. Steinmeier ametumia fursa ya mazungumzo hayo kutowa wito kwa Karzai kusaini haraka makubaliano ya usalama na Marekani ambayo yangelitowa kinga ya kutoshtakiwa nchini humo kwa wanajeshi wa kigeni watakoendelea kubakia nchini humo baada ya mwaka 2014.

Amesema jambo hilo ni muhimu kuhakikisha kwamba wanajeshi hao wanabakia nchini humo kama wakufunzi baada ya kuondolewa kwa vikosi vya mapigano.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na waziri mwenzake wa Afghanistan Zarar Ahmad Osman katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kabul. (09.02.2014).

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na waziri mwenzake wa Afghanistan Zarar Ahmad Osman katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kabul. (09.02.2014).

Akizungumza kabla ya kukutana na Karzai katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na waziri mwenzake wa Afghanistan Sarar Ahmad Osmani, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ameeleza kwamba "mpango wa mchakato" ni muhimu hata kwa jeshi la Ujerumani.Amesema hilo sio jukumu unaloweza kuliandaa kwa siku 14, bali wanahitaji muda kuusadikisha umma na bunge juu ya mchakato huo.

Baraza la mawaziri la serikali ya shirikisho hapo Jumatano limeongeza muda wa mwisho wa miezi kumi kwa operesheni za mapigano za jeshi la Ujerumani za miaka 12 nchini Ufghanistan. Bunge la Ujerumani "Bundestag" linatazamiwa kuamuwa juu ya suala hilo hapo Februari 21 na inatarajiwa kuidhiniskwa kwa kauli moja.

Kuanzia mwakani Ujerumani itabakisha wanajeshi kati ya 800 na 600 kutowa mafunzo na ushauri kwa jeshi la Afghanistan.Zaidi ya wanajeshi 3,100 wa Ujerumani hivi sasa wanatumika nchini Aghanistan na wakati wa kilele wa operesheni zao walifikia wanajeshi 5,350.Wanajeshi 55 wa Ujerumani wameuwawa wakiwa Afghanistan.

Ziara ya Steinmeier nchini Afghanistan haikutangazwa hadharani kwa sababu za usalama.

Mwandishi: Mohamed Dahmn/AFP,dpa,Reuters

Mhariri: Amina Abubakar

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com