1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arsenal walipiza kisasi kwa Man United

11 Machi 2019

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solksjaer alipata kipigo chake cha kwanza katika ligi Jumapili tangu achukue mikoba kutoka kwa Jose Mourinho, pale timu yake ilipofungwa magoli mawili bila jawabu.

https://p.dw.com/p/3EnH6
Fußball Champions League Manchester United - Paris St. Germain
Picha: Reuters/J. Cairnduff

Granit Xhaka na Pierre Emerick Aubameyang ndio waliowafungia Arsenal mabao yao na kuwafanya wawapiku United katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo. Huyu hapa Solksjaer.

"Lazima uvunjwe moyo na matokeo haya, lakini tumecheza mchezo mzuri. Tulibuni nafasi nzuri kuliko tulipowashinda kwenye kombe la FA. Bila shaka goli la kwanza ndilo linaloamua jinsi mchezo utakavyokwenda," alisema Solksjaer.

Mechi hiyo ilikumbwa na kisa cha shabiki wa Arsenal kuingia uwanjani na kumsukuma beki wa United Chris Smalling jambo lililolaaniwa sana huku wengi wakitaka hatua zaidi za kuwalinda wachezaji zichukuliwe baada ya kisa hicho kuwa cha pili hapo Jumapili tu, baada ya shabiki wa Birmingham City kumshambulia nahodha wa Aston Villa Jack Grealish kwenye mechi ya ligi ya daraja la kwanza. Unai Emery ni kocha wa Arsenal.

"Sipendi kitu kama hicho kinapotokea lakini hakiko kwenye udhibiti wangu. Nafikiri tunafurahia uungaji mkono tunaopata kwa kila shabiki, lakini nafikiri wanastahili kushabikia kwa heshima," alisema Emery.

Kwa sasa Manchester City waliowafunga Watford tatu moja Jumamosi ndio vinara wakiwa na pointi 74 Liverpool wanawahemea kooni wakiwa na pointi 73 halafu Tottenham Hotspur, Arsenal, Manchester United na Chelsea wote wanawania nafasi ya tatu na ya nne.