Siku DW iliponikutanisha na baba yangu | Miaka 50 ya DW Kiswahili | DW | 16.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Miaka 50 ya DW Kiswahili

Siku DW iliponikutanisha na baba yangu

"Aliposikia hilo jina la mama yangu, ghafla akageuka kuniangalia kwa mshangao na butwaa. Macho yake yalionesha kutoamini alichokisikia. Alikuwa kama mtu aliyekumbushwa hadithi ya zamani..." - Hadithi ya kubuni

Wettbewerb zum 50-jährigem Jubiläum. Ayoub Kimweli +255652192421 AyoubKimweli@yahoo.com

50 Jahre Kisuaheli Redaktion Wettbewerb

Ilikua yapata saa 7:15 mchana, nilipofungua redioa yangu na kusikia ripoti hii:

“Kundi la waasi la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, limesema linabadili jina la tawi lake la kijeshi na linajiandaa kuzima mashambulizi mapya dhidi yake. Kwa mujibu wa kiongozi wa kundi hilo, sasa tawi la kijeshi la kundi hilo litajulikana kama Jeshi la Ukombozi na kwamba kamanda wake wa kijeshi, Kanali Mavunga Shukurani, amepandishwa cheo kuwa jenerali...." Mtuma ripoti akamalizia kwa kujitambulisha: "Mimi ni John Kanyunyu, Deutsche Welle, Goma."

Pheww!!! Nikaachia pumzi nilizokua nimezizuia kwa nguvu mithili ya mtu aliyemekabwa koo kwa muda mrefu. Pangelikuwa na mtu karibu yangu, lazima angelipigwa na butwaa. Ghafla ile moja, akili yangu ikakosa uhusiano na kiwiliwili. Nikajigundua nimechuruzikwa na haja ndogo bila kujitambua.

Rundo la mawazo liliendelea kuumiza kichwa changu. Nikaamua kwenda kulala, ingawa bado kungali mchana na jua la Kigoma, Tanzania, lilikuwa linawaka kama limekula yamini. Sikumbuki saa ngapi hasa hatimaye usingizi uliponichukua, maana nilipoteza muda mrefu sana nikiwaza na kuwazua, ila nakumbuka kuwa nilipoamka, tayari jioni ikianza kuingia, maneno ya marehemu mama yangu mzazi yalinijia kichwani:“Ukikua, tafuta kila njia uonane na baba yako umpe huu ujumbe.''

Nikakurupuka kukimbilia kabati langu la nguo na humo nikaitwaa ile ile bahasha niliyopewa na marehemu mama. Sikuwahi kuisoma tangu aliponipa kabla ya kifo chake miaka 18 iliyopita. Ila siku hiyo uvumilivu ulinishinda. Nikaifungua huku mikono ikitetemeka na jasho jembamba likinitoka.

Moyo wangu ulikua unadunda kwa hofu, lakini sauti nyembamba ndani yangu ilinisukuma kufungua. Ilikuwa sauti ya mama. Nina hakika, ilikuwa sauti yake. Mboni za macho yangu zilifunguka mpaka mwisho na maneno machache yaliyoandikwa kwa muandiko wa mkono wa mama. Yalisomeka kama maji:

Shukurani,

Huyu ndio yule mtoto uliyemkataa tulipokuwa Kigoma. Nimemtuma kwako umuone, lakini pia naomba umpatie kile kidani changu ulichonipokonya kipindi kile. Naomba kwa moyo wangu wote, kwani kidani hicho ndio urithi pekee niliomuachia mwanangu. Sikuwa na mali wala uwezo wa kumpatia elimu. Nakuomba sana Shukurani.

Ni mimi niliekupenda sana,

Maimuna Mamu.''

Machozi mengi yakanitoka. Uchungu mkubwa ukauvamia moyo wangu. Maswali mengi yakaendelea kuuzonga ubongo wangu. Mengi sikuwa na hakika nayo, tangu mama yangu alipofariki dunia na kuniwacha mtoto mdogo wa miaka minane hadi sasa. Hata hii barua sikuwahi kuipa maana kwenye maisha yangu ya kuhangaika na kukua kwa kupenyapenya.

Na hadi hivi sasa nilipokuwa ndio kwanza nimeisoma, sikuwa na hakika na chochote kile, lakini baada ya kuisoma nikajua kwamba nilitaka kuupata huo urithi alioniachia mama yangu, Maimuna. Kidani!

Ni hamu ya hicho kidani ndiyo iliyonipa ujasiri wa kujifuta machozi na kuanzia hapo nikaanza kupanga na kupangua namna ya kumfikia huyo Shukurani, ambaye kwa maneno ya mama kwenye barua ile, ndiye baba yangu. Na ndipo sasa nikagundua maana ya kupatwa na hisia zile kali, baada ya kusikiliza ripoti ya DW kutoka kwa John Kanyunyu wa Goma, mashariki ya Kongo, ambayo ilimtaja kamanda wa waasi wa M23, Mavunga Shukurani.

Haikuwa mara yangu ya kwanza maishani kulisikia jina hilo, lakini ilikuwa mara ya kwanza hisia zangu kuchotwa nalo. Na hisia hazidanganyi, ndivyo mama alivyokuwa akiniambia. Kufika hapo nikawa nimeshaamua kumtafuta Shukurani aliyetajwa na DW kwa udi na uvumba hadi nimtie yeye au anitie mimi mikononi. Tutiane mikononi, maana mimi naye tu wa damu moja!

Uwezo wangu kifedha haukuwa mkubwa kuniruhusu kufunga safari kuelekea Goma, lakini hata kama ningelifika huko, sikuwa nafamu ni kwa jinsi gani ningelimuona mtu ambaye sasa amekuwa jenerali wa kundi la waasi, anayetafutwa na serikali kwa uadui na anayefuatwa na wapiganaji wake kwa imani.

Lakini nikajipa moyo, kila sura ya mama yangu iliponijia kichwani, maneno yake nikayasikia kwenye kimya cha usiku na sura ya kidani nisichokijua nikiiota ndotoni, nikawa na imani kwamba kuna siku isiyo jina nitakutana uso kwa uso na mwenye urithi pekee kutoka kwa mama yangu.

Siku, wiki na miezi ilipita huku nikibaki kuwa msikilizaji wa kudumu wa vipindi vyote vya Deutsch Welle. Mungu si Athumani, baada ya takribani mwaka mmoja kupita, siku moja saa 12:16 jioni masikio yangu yakakumbana na kile nilichokuwa nakitafuta. Ilikuwa tena sauti ya John Kanyunyu akiripoti kutokea huko huko Goma, mashariki mwa Kongo, ingawa ripoti yenyewe niliipata mwisho mwisho:

".... huku hayo yakiendelea, mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kamanda Mkuu wa majeshi ya waasi wa mashariki ya Kongo, Jenerali Mavunga Shukurani, yatakayofanyika wiki mbili zijazo nje kidogo ya mji wa Goma, yanategemewa kuleta ufumbuzi wa mgogoro huu wa miezi 18 sasa”

Kwangu cha muhimu hayakuwa hayo mazungumzo ya baina ya waasi na serikali. La hasha! Bali ni matumaini ya kuweza kuitumia nafasi hiyo kuonana na Shukurani, baba yangu, na kumfikishia ujumbe nilioachiwa na Maimuna, mama yangu.

Ndani ya wiki mbili hizo nilijitahidi kufanya kazi kwa bidii na kuweka vizuri kila senti niliyoipata. Hakuna mtu niliyemwambia siri iliyo moyoni mwangu, na siku niliyowaaga marafiki zangu kuwa sasa nakwenda Kongo, walinishangaa sana.

Wengi walinishauri nisiende, akiwemo mpenzi wangu, Naitovwaki, ambaye aliumia sana moyoni. Aliamini kwamba hiyo ingelikuwa mara yake ya mwisho kuniona, maana huko nilikokuwa nakwenda, watu wanakukimbia kutokana na vita na mateso yake. Lakini nilikuwa nimedhamiria na kusingelikuwa na lolote la kuirudisha nyuma dhamira yangu. Hata moja!

Siku ya siku ikafika. Nilijichomeka katika ya kundi la waandishi wa habari wanaokwenda Kongo kufuatilia mazungumzo ya serikali na waasi na pia kuripoti juu ya mapigano. Huku nikijidai kuwa ni mmoja wao, nilitumia simu yangu kama kifaa cha kunasia sauti ili kuwababaisha maafisa wa usalama na waandishi wasinijuwe.

Muda wa kusikiliza Deutsche Welle haukunifanya kuwa mwandishi wa habari, lakini ulinipa maarifa mengi juu ya fani hiyo. Hatimaye niliingia Goma, nikafika hadi kwenye eneo ambalo linatambuliwa kama "salama" kwani majeshi ya serikali na ya waasi yalikuwa yametenganishwa na ya Umoja wa Mataifa. Hapo ndipo palipokuwa na hoteli ambayo wajumbe wa serikali na waasi walikuwa wanakutana kufanya mazungumzo.

Hapo waandishi wengi walikuwa wanasukumana kukusanya taarifa na ripoti. Mminyano ulikuwa mkali, kila mwandishi wakitaka kupata picha na sauti kutoka kwenye mazungumzo hayo.

Kwa bahati mbaya nilimkanyaga dada mmoja mnene na mfupi wa kimo, lakini kwa kuwa mimi ni Mtanzania nikawahi kumuomba msamaha. Alinishangaa sana na akasema maneno ya Kifaransa ambayo kamwe sikuyaelewa maana yake. Mara akaniambia kwa Kiswahili kibovu kuwa nimsaidie kuuliza swali pindi Jenerali Shukurani atakapotokea. Kwangu ulikuwa mtihani mkubwa kwani kwanza, mimi sikuwa mwandishi wa habari, na pilia huyo Jenerali Sultani mwenye sikuwa namfahamu, ingawa ndiye aliyenifanya kufunga safari hii kutokea Kigoma, Tanzania.

Mara watu watatu warefu wakatokea kutoka kwenye chumba cha mazungumzo na kila mmoja kati yetu alikuwa akihaha kupata picha na kutaka kuwahoji watu hao.

"Yupi kati ya hawa ndiye Jenerali Shukurani?", nikamuuliza yule mwandishi habari wa kike niliyemkanyaga mwanzoni.

Akanionyesha kwa kidole, nami nilijitahidi kuminyana ili nipate nafasi ya kumpiga picha na kumuuliza swali langu na la swali la yule dada.

Kwa kweli nilijitahidi kwa nguvu zangu zote na nilipiga kelele kwa Kiswahili “nichague mimi, nichague mimi, nichague mimi.'' Jenerali na wenzake walikua wameshaanza kuondoka. Nikalimbilia gari lao nikiita kwa nguvu: “Jenerali Shukurani, Jenerali Shukurani. Naomba nisikilize. Nina ujumbe wako kutoka kwa Maimuna Mamu wa Tanzania.”

Aliposikia hilo jina la mama yangu, ghafla akageuka kuniangalia kwa mshangao na butwaa. Macho yake yalionesha kutoamini alichokisikia. Alikuwa kama mtu aliyekumbushwa hadithi ya zamani, ambayo alikuwa muhusika wake lakini pia akawa si sehemu yake. Katikati ya mshangao wake, nikapatiza kumpa ile bahasha, naye haraka haraka akaitoa karatasi iliyokuwamo ndani yake na kuisoma kwa kimoyomoyo.

Nilikuwa natetemeka kwa hofu na kusubiri kwa makini. Alipomaliza kusoma aliniangalia mara moja, halafu akataka kuondoka, lakini kisha kama mtu aliyebadilisha mawao ghafla akaniambia kwa Kiswahili kizuri: "Naomba upande kwenye gari tukaongee nyumbani." Mara wasaidizi wake walinipandisha garini, tukaanza kuondoka.

Nilipoingia kwenye gari tu, ghafla mlinzi mmoja alinibana mikono na mwingine alinifunga kitambaa machoni, midomoni mwangu walishindia fusho la vitambaa. Nikadhania kuwa mwisho wangu ndio umekaribia na hivi punde nitamfuata mama yangu, Maimuna huko aliko.

Gari iliyotubeba ilizunguka sana lakini hatimaye tulishuka kwenye gari na kutembea kama tunashuka ngazi hivi. Niliamriwa nikae chini na wakaanza kunifungua. Waliponifungua kile kitambaa cha machoni, nilikutana uso kwa uso na Jenerali Shukurani, baba yangu. Akawaamuru wale wasaidizi wake waondoke wote. Nikabaki mimi na yeye. Baada ya yote yaliyokwishatokezea, sikuwa tena na hofu yoyote ile. Nilikuwa tayari na lolote ambalo lingenitokezea.

Lakini kitu chenyewe kilichotokezea, sikuwa nimekitarajia. Badala ya kunizaba vibao na kunikana, Jenerali Shukurani aliniuliza tu maswali mengi kwa upole na kwa udadisi. Mwishowe akapiga magoti mbele yangu kuniomba msamaha kwa yote yaliyotokea. "Nisamehe mwanangu."

Tulikumbatiana kwa muda mrefu, huku machozi yakitutiririka. Hatimaye akatia mkono mfukoni mwa magwanda yake ya kijeshi na akanikabidhi kile kidani alichoambiwa na mama. Kilikuwa kama kipya, na cha dhahabu tupu. Nilikuwa na maswali mengi ya kumuuliza, lakini hisia nzito ziliujaza ulimi wangu mdomoni, zaidi ya "Ahsante baba'angu", sikuwa na jengine nililoweza kulisema.

Akaninasihi sana nibaki japo kwa siku moja pamoja naye. Nilikubali na baada ya siku mbili niliaga na kuanza safari kurudi nyumbani Tanzania.

Mpaka leo nasimulia haya nikiwa mwenyewe siamini kilichotokezea. Sikuwahi kumsimulia mwengine yeyote mkasa huu hadi hivi leo. Heko Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle kwa kutimiza miaka 50 na kunisaidia kukutana na baba yangu.

Tanbihi: Hii ni hadithi ya kubuni iliyoandikwa na Amon Tamilwa wa Dar es Salaam, Tanzania na picha imechorwa na Ayoub Kimweli kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle.

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com