1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sierra Leone imejifunza nini baada ya vita vya miaka 11?

Amina Mjahid
18 Januari 2022

Vita vibaya vya wenyewe kwa wenyewe Afrika vilimalizika miaka 20 iliyopita Sierra Leone. Kwa miaka 11 ya vita, maelfu ya watu waliuwawa, wengine wakaitoroka nchi na wengine kupitia mateso huku miundo mbinu ikiharibiwa.

https://p.dw.com/p/45g85
Sierra leone | Strassenszene in Freetown
Picha: Ute Grabowsky/photothek/picture alliance

Miaka 20 baada ya vita hivyo suali linaloulizwa ni je Sierra Leone imefikia wapi katika upatikanaji wa amani na maridhiano? Tume ya ukweli na maridhiano iliochunguza sababu za vita hivyo ilipendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuzuwia kutopatikana kwa haki, kuzuwia ubaguzi kwa misingi ya kikabila, kimaeneo na kisiasa na hata ufisadi. Miaka 20 baadae watu wanakumbuka historia kwa machungu, wanaangalia hali iliyoko sasa na siku zao za usoni kwa hisia mseto.

Theophilus Gbenda, Mwanaharakati anayepigania amani, anasema alipoteza jamaa zake na baadhi ya nyumba zao zilichomwa moto. Anasema cha kusikitisha ni kwamba taifa hilo bado halijajifunza mengi kutokana na historia yake iliyojaa umwagikaji damu.

"Nilipoteza watu, nyumba zetu zilichomwa moto na chifu wa eneo letu aliuwawa mbele ya mke wake na watoto. sote tulijua kilichosababisha vita. ukiangalia kile Sierra Leonne ilichojifunza  tangu kumalizika kwa vita hivyo ni kama hatujajifunza chochote Maana mambo yaliyosababisha vita  kama ufisadi, ukabila, utawala mbovu, ukosefu wa haki na umasikini haya yote bado yapo nasi."

Takriban kila familia Sierra Leone ina simulizi ya kusikitisha ya miaka 11 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tume ya kupambana na ufisadi ya Czar ni moja ya tume zilizopitia mengi katika vita hivyo. Tume hiyo inayoongozwa na Francis Ben Kaifala ilipendekezwa na tume ya ukweli na maridhiano. 

"Miaka 10 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ni wakati tuliyopitia mengi magumu. Tuliona uhalifu ukifanywa na binaadamu kwa binaadamu. Cha kusikitisha ni kwamba mambo haya yalifanywa na raia wetu dhidi ya watu wake wenyewe. Watu walikatwa miguu, kwa miaka kadhaa watu hakuwenda mashuleni. niliyashuhudia haya kabla hatujaondoka kukimbilia Guinea. Najua tukiangalia tulikotoka tunajua sote kwamba vita sio vizuri na tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuviepuka," alisema Francis Kaifala

Mambo aliyoyapitia wakati wa vita hivyo huenda ikawa ndio sababu ya kutoa wito wa kuundwa taasisi za kitaifa zilizothabiti. Kaifala anasema kuna mapendekezo mengi yaliowekwa ili kuhakikisha sierra leone hairejei ilipotoka. Lakini pia kuna mambo mengi yaliyosababisha vita hivyo kama ukabila, ambayo pole pole yameanza kushuhudiwa tena. Francis Ben Kaifala anasema taasisi kama Polisi na mahakama zinapaswa kujisimamia na kuwa na maamuzi yake yenyewe huku akisisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa.

Kuna baadhi ya watu wanaoona Sierra leone imefanya kazi nzuri ya kuiponya nchi kutokana na makovu ya vita na kusonga mbele na hiyo inawapa wengi matumaini ya Sierra Leonne wanayoitaka. Fatmatta Kamara ni muandishi nchini humo anasema taifa limetoka mbali na limefanikwa kuandaa chaguzi zilizokuwa na amani, kuna taasisi zilizoundwa ili kukuza utawala bora na bado kuna juhudi zinazofanywa ili kuimarisha sekta ya elimu pamoja na usalama. Fatmatta anasema kwake anaona maenedeleo kwa takriban kila sekta Sierra Leone.

Mwandishi: Claudia Anthony/Amina Abubakar