Sheria dhidi ya maandamano yaanza kazi Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Sheria dhidi ya maandamano yaanza kazi Ukraine

Licha ya lawama za mataifa ya Magharibi na upinzani, sheria inayopiga marufuku maandamano nchini Ukraine imeanza kazi rasmi, huku makabiliano kati ya waandamanaji na polisi kwenye mjini Kiev yakiingia siku yake ya tatu.

Waandamanaji mjini Kiev wakikabiliana na polisi.

Waandamanaji mjini Kiev wakikabiliana na polisi.

Sheria hizo mpya, ambazo zinakataza karibu aina zote za maandamano, zimechapishwa kwenye gazeti la bunge la Ukraine, Golos Ukrainy, baada ya onyo la Rais Viktor Yanukovych kwamba ghasia zinatishia usalama wa nchi nzima.

Sheria hizo zinatoa adhabu ya kifungo cha hadi miaka mitano kwa wale wanaoweka vizuizi kwenye majengo ya serikali na ruhusa ya kuwakamata waandamanaji wanaoziba nyuso zao au kuvaa kofia za chuma. Vifungu vyengine vya sheria hizo vinapiga marufuku usambazaji wa "kashfa" mitandaoni.

Mjini Kiev kwenyewe, mapambano ya juzi na jana, yameugeuza mji huo kuwa uwanja wa kivita, huku kiasi cha waandamanaji 10,000 wakipambana na vyombo vya usalama.

Waandamanaji hao wanaripotiwa kuendelea kukaidi amri ya polisi inayowataka watawanyike, na usiku mzima wa kuamkia leo ulishuhudia mapambano kwenye mitaa ya mji huo, ambapo licha ya polisi kufanikiwa kuondosha baadhi ya vizuizi vilivyowekwa na waandamaji, waandamanaji hao waliweza kuwarudisha nyuma polisi hadi kwenye eneo walilokuwa awali.

Serikali yasmea haitumii nguvu

Maandamano yalipogeuka moto usiku wa tarehe 20 Januari 2014.

Maandamano yalipogeuka moto usiku wa tarehe 20 Januari 2014.

Hata hivyo, msemaji wa wizara ya ndani, Serhiy Burlakov, amesema polisi wameendelea kutotumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji.

"Polisi wanajiepusha kabisa na kutumia nguvu kwa sababu tunafahamu kwamba waandamanaji wanatuchokoza kusudi tuingie kwenye ghasia." Alisema Burlakov.

Upinzani umeituhumu serikali kwa kuwalipa wahuni kuvunja vioo na kuchoma moto magari ili kuyafanya maandamano yao yaonekane ya fujo.

Mapambano hayo yalianza baada maandamano ya watu wapatano 200,000 dhidi ya sheria hizo kali zinazopiga marufuku maandamano kupitishwa bungeni na wafuasi wa Rais Yanukovych siku ya Jumapili.

Katika hotuba yake kwa taifa hapo jana kupitia televisheni, Rais Yanukovych alionya kwamba ghasia zinatishia kuibomoa misingi ya taifa zima, ambalo limegawika kati ya wale wanaounga mkono Ulaya na wale wanaoiunga mkono Urusi.

Yanukovych alisema uvumilivu wake kwa hali hiyo unazidi kupungua, ingawa alionesha utayarifu wa kuzungumza na upinzani. Hata hivyo, kiongozi wa upinzani, Arseniy Yatsenyuk, amesema watashiriki kwenye mazungumzo kwa masharti maalum.

"Kwanza, idhini ya kufanya mazungumzo hayo itoke Maidan, pili mazungumzo hayo yawe ya wazi kwa umma, na tatu mazungumzo hayo yawe hatua ya kwanza tu kuelekea kwenye kukidhi matakwa yetu." Aliyataja masharti hayo.

Kiongozi mwengine wa upinzani, Vital Klitschko, amesema watazungumza tu na serikali, ikiwa tu Rais Yanukovych atahudhuria mwenyewe kwenye mazungumzo hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com