Shambulio la kujitowa muhanga lauwa zaidi ya watu 100 Iraq | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Shambulio la kujitowa muhanga lauwa zaidi ya watu 100 Iraq

Shambulio la kundi la Dola la Kiislamu kwenye soko lililofurika watu katika jimbo la mashariki la Diyala limeuwa watu 115 wakiwemo wanawake na watoto katika shambulio baya kabisa katika kipindi cha muongo mmoja.-

Shimo lililosababishwa na mripuko Diyala, Iraq. (18.07.2015)

Shimo lililosababishwa na mripuko Diyala, Iraq. (18.07.2015)

Wahanga ambao wengi walikuwa ni Washia walikuwa wamekusanyika kuadhimisha kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao umemalizika Ijumaa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na siku moja kabla kwa wenzao wa madhehebu ya Sunni.

Polisi imesema lori dogo liliripuliwa kwenye soko hilo hilo lililojaa watu katika mji wa Khan Beni Saad Ijumaa ambapo mara moja sherehe ziligeuka kuwa maafa huku vipande vya miili vikiwa vimetawanyika kila mahala katika soko hilo.Maafisa wa polisi wanasema takriban watu 170 wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Mkaazi wa Diyala Sayif Ali amekaririwa akisema "Khan Beni Saad imekuwa eneo la maafa kutokana na mripuko huo mkubwa kabisa."Ameendelea kusema kwamba "Hii ni siku ya kwanza ya Eid,mamia ya watu wameuwawa, wengi wamejeruhiwa na bado tunaendelea kutafuta miili zaidi."

Shambulio latonesha mzozo wa madhehebu

Eneo la mripuko Diyala, Iraq.(18.07.2015)

Eneo la mripuko Diyala, Iraq.(18.07.2015)

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio hilo katika taarifa iliowekwa kwenye mtandao wa Twitter wenye uhusiano na kundi hilo la wanamgambo.

Spika wa bunge la Iraq Salim al- Jabouri amesema Jumamosi kwamba shambulio hilo limetonesha vibaya mzozo wa madhehebu na kwamba serikali inajaribu kulidhibiti kundi hilo la kigaidi la Daesh kama linavyoiitwa kwa jina la Kiarabu lisiliyumbishe jimbo la Diyala.

Lakini ghadhabu imechemka katika jimbo hilo tete ambapo miji yake kadhaa ilitekwa na kundi hilo la Dola la Kiislamu mwaka jana.Vikosi vya Iraq na wapiganaji wa Kikurdi tayari wameyakombowa maeneo hayo lakini mapambano kati ya wanamgambo na vikosi vya usalama bado yanaendelea.

Mkaazi mwengine wa Diyala akizungumza kwa sharti ya kutotajwa jina kwa kuhofia kisasi amesema walikuwa wamekwenda kwenye soko hilo kufanya manunuzi na kujiadaa kwa ajil ya siku kuu hiyo ya Eid ili kuipokea kwa uchangamfu lakini furaha hiyo iligeukwa kuwa majonzi kwa kupoteza familia, marafiki na jamaa yote kwa sababu ya serikali kushindwa kuwapatia usalama.

Usalama waimarishwa

Eneo la mripuko Diyala, Iraq.(18.07.2015)

Mwanajeshi wa Iraq,

Vikosi vya usalama vimemwagwa kwa wingi hapo Jumamosi na kuwekwa mara moja kwa vituo vipya vya ukaguzi pamoja na kuanzishwa kwa taratibu za usalama katika jimbo hilo.

Kundi hilo la wanamgambo wa Kisunni limekuwa likihusika na mashambulizi kadhaa makubwa dhidi ya raia au vituo vya ukaguzi wakati likiwa katika harakati zao za kujitanuwa. Kundi hilo hivi sasa linadhibiti kama theluthi moja ya Iraq na Syria eneo ambalo wamejitangazia kuwa la ukhalifa la utawala wa Kiislamu.

Hapo mwezi wa Augusti mwaka jana takriban watu 64 wameuwawa katika shambulio kwenye msikiti wa Wassuni katika jimbo hilo la Diyala kwa kile wakaazi wa eneo hilo wanachoamini kuwa lilikuwa ni shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya watu wa makabila waliyokataa kutangaza utii wao kwa kundi hilo la Dola la Kiislamu.

Mashambulizi ya anga

Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.

Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.

Marekani imekuwa ikitumia mabilioni kulipatia silaha na mafunzo jeshi la Iraq lakini halikufanya vizuri mwaka jana wakati vilipotimuliwa na kundi la Dola la Kiislamu waliokuwa wakiteka maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Iraq.Muugano unaongozwa na Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na kundi hilo la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria tokea mwaka jana lakini mashambulizi hayo yameshindwa kuzuwiya kusonga mbele kwa kundi hilo.

Wanamgambo hao hivi karibuni waliuteka mji wa Ramadi katika jimbo la magharibi la Iraq la Anbar na mji wa kale wa Palmyra nchini Syria.

Jimbo la Diyala ambalo linapakana na Iran ni jimbo pekee nchini Iraq ambapo ndege za kivita za Iran zimefanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo mapema mwaka huu.Serikali ya jimbo la Diyala imetangaza siku tatu za maombolezo.

Mwandishi : Mohamed Dahman / AP/Reuters

Mhariri : Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com