Serikali Sudan Kusini leo wameanza mazungumzo ya amani na waasi | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali Sudan Kusini leo wameanza mazungumzo ya amani na waasi

Viongozi wa Serikali na waasi nchini wa Sudan Kusini leo wameanza rasmi mazungumzo ya kutafuta suluhu dhidi ya mvutano wao wa kisiasa uliopelekea mapigano na kusababisha vifo vya watu wengi.

Raia wa Sudan Kusini waliokimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika ofisi za umoja wa mataifa mjini Juba

Raia wa Sudan Kusini waliokimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika ofisi za umoja wa mataifa mjini Juba

Mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika kwa wiki tatu mfululizo mjini Adis Ababa Ethiopia, na pia kuhudhuriwa na ujumbe wa viongozi kadhaa kutoka mataifa ya ukanda huo.Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia, imethibitisha kuanza kwa mazungumzo hayo mjini Adis Ababa, na kuongeza kuwa shirika la ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika, IGAD limeahidi kusaidia kufanikisha mazungumzo hayo kwa kadri iwezavyo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo hayo,Hilde Johnson, amesisitiza kuzingatiwa kwa upatanishi na kumaliza tofauti kati ya pande hizo mbili kwa kusameheana kutokana na machungu yaliyosababishwa na miutano yao ya kisiasa kwa kushirikisha makabila makuu mawili ambayo ni kabila la wa Dinka linalomuunga mkono rais Salva Kiir, na kabila la Nuer linalomuunga mkono Riek Machar.

Mmoja wa wanajeshi wa Serikali ya Sudan kusini mbele ya bunduki aina ya mashine gun katika mji wa Malakal

Mmoja wa wanajeshi wa Serikali ya Sudan kusini mbele ya bunduki aina ya mashine gun katika mji wa Malakal

Aidha waangalizi wengine wa masuala ya kisiasa wanashauri mazungumzo hayo ni vema yaanze kesho baada ya wahusika kuwasili leo, kwa kuwa wameamua kukutana kwa ajili mya kuleta suluhu na kutafuta amani ya raia wao, ingawaje kwa mujibu wa tamko la serikali ya Sudan Kusini lililotolewa siku ya alhamisi, ni kwamba waasi bado hawapo tayari kumaliza uhasama huo.

Mapigano mengine yazuka Bor

Wakati mazungumzo hayo ya kutafuta suluhisho la migogoro ya kisiasa ya Sudan Kusini yanatarajiwa kuanza leo, lakini bado vurugu zinaenedelea, ambapo jeshi la nchi hiyo kwa kwa mara ya pili sasa wanafanya jitihada za kurejesha mji wa Bor kutoka kwa waasi walioushikilia.

Kufuati milipuko inayoendelea katika mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya waasi, kumesababisha afisa wa ngazi ya juu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa mataifa, Toby Lanzer, kutoa onyo kwa vikosi hivyo vya pande mbili kuacha mapigano haraka na kuwajibika katika kulinda usalama wa raia wao na mashirika yanayosaidia kutoa misaada kwa wahanga wa mapigano hayo, na kusema kuwa kinyume na hayo, wanasababisha mazingira ya kusaidia kuwa magumu zaidi.

Toby Lanzer aliongeza kuwa, Mapigano yaliyozuka nchini humo mwezi Desemba,na kudumu kwa wiki tatu mfululizo, yalisababisha idadi ya watu takriban laki 2 kukimbia makazi yao na kuathiri wengine.

Mmoja wa askari wa Umoja wa Mataifa akiwasili katika uwanja wa ndege wa Juba nchini Sudan

Mmoja wa askari wa Umoja wa Mataifa akiwasili nchini Sudan

Maelfu ya watu wamekuwa wakikimbia baada ya milipuko kuzuka tena, kwa kukimbilia nchi jirani, ambapo wengine wamekuwa wakikimbialia kuelekea maeneo jirani kwa kuvuka mto Nile, kwa kutumia mashua za kawaida.

Mapema wiki hii Rais Kiir, alisema kuwa, vita havina maana yoyote ingawa hayupo tayari kugawana madaraka na waasi, na kuwakanya waasi kwa tamko alilolitoa kupitia BBC kuwa iwapo wanataka kuingia madarakani hawapaswi kufanya uasi kwa kuchukua madaraka.

Marekani kuondoa watu wake wote Sudan Kusini

Hivi sasa Marekani imeondoa wafanyakazi wake wote waliokuwepo mjini Juba nchini humo, na kusema kuwa hali ya machafuko inayoendelea si salama kwa raia wake kuendelea kuwepo nchini humo.

Machafuko nchini humo yalilipuka tarehe 15 mwezi Desemba mwaka jana, lilipotokea jaribio la kuipindua serikali ya rais Kiir, ambapo rais Kiir alimshutumu Riek Machar kuhusika na mpango huo kumpindua dai ambalo Machar amelikanusha.

Mwandishi: Diana Kago/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com