Serikali na Renamo waafikiana Msumbiji | Matukio ya Afrika | DW | 25.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Serikali na Renamo waafikiana Msumbiji

Serikali ya Msumbiji na kundi la waasi la Renamo chama kikuu cha upinzani, wametia saini makubaliano ya kumaliza vita vyao vya takriban miaka miwili.

Rais Armando Guebuza na kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama

Rais Armando Guebuza na kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama

Mpango huo umetiwa saini baada ya kuwa na majadiliano marefu yaliyosimama kufuatia matakwa ya kundi la Renamo kujumuishwa katika jeshi la nchi hiyo.

Masuala hayo kwa sasa yamewekwa kando, lakini bado yanatarajiwa kushughulikiwa wakati waangalizi wa kimataifa watakapojitayarisha kuongoza kipindi cha kuweka silaha chini kwa kundi hilo.

Bendera ya chama tawala Frelimo

Bendera ya chama tawala Frelimo

Renamo ni vuguvugu la waasi wa zamani waliotiliana saini makubaliano ya amani na chama kinachotawala cha Frelimo mwaka wa 1992 na kumaliza muda mrefu wa umwagikaji wa damu uliosababisha kuondola kwa utawala wa mkoloni Ureno kutoka katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.

Renamo sasa ni kundi kubwa la upinzani lililo na wanachana 51 katika bunge la wanachama 250 nchini humo. Hata hivyo makubaliano hayo yaliotiwa saini na wakuu wa pande zote mbili yanatarajiwa kutiwa saini na rais Armando Guebuza na kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama katika sherehe itakayofaynika hadharani.

Aidha Dhlakama amekuwa akijificha katika eneo la kati la milima ya Gorongosa. Mpaka sasa haijawa wazi iwapo atapambana na Rais Guebuza katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15.

Kibarua kigumu chamsubiri mshindi wa uchaguzi mkuu ujao

Mambo yatakayokuwa katika mpango huo wa amani yalitangazwa hivi karibuni, ambapo msahama uliidhinishwa kwa kundi hilo wiki mbili zilizopita hali itakayompa nafasi kiongozi wa Renamo Dhlakama kuondoka eneo analojificha na labda kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama

Kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama

Kwa upande mwengine katiba ya nchi hiyo haimpi nafasi rais Guebuza kuwania tena kiti cha urais kwa kipindi cha tatu kwa hiyo aliyekuwa waziri wa Ulinzi Filipe Nyusi ndiye atakayewania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Frelimo.

Yeyote atakayeshinda katika uchaguzi huo atakabiliwa na kibarua kigumu cha kufufua mipango ya uwekezaji ya mkaa wa mawe na gesi inayozalishwa kwa wingi nchini humo ili kuimarisha uchumi wa nchi hiyo. mipango hiyo iliharibiwa miongo miwili iliopita kufuatia msukosuko uliokuwepo.

Vita vya chini kwa chini vilivyokuwa vinaendelea kati ya wanajeshi wa serikali, Polisi na kundi la upinzani Renamo kuanzia mwaka wa 2012 vilizua hofu ya kurejea tena mapambano makali yaliokuwepo kuanzia mwaka wa 1975 hadi mwaka wa 1992 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFPE/AFP

Mhariri:Josephat Charo