Sera ya misaada ya Ujerumani yakosolewa | Masuala ya Jamii | DW | 18.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Sera ya misaada ya Ujerumani yakosolewa

Taasisi za misaada za Ujerumani zimezindua ripoti iliyopewa jina la "Ukweli wa Sera za Maendeleo" inayokosoa ukosefu wa dhana ya ushirikiano wa pamoja katika sera ya maendeleo ya Ujerumani.

Waziri wa Maendeleo, Dirk Niebel.

Waziri wa Maendeleo, Dirk Niebel.

Ujerumani ni ya pili duniani kwa kutoa misaada ya maendeleo, baada ya Marekani. Katika orodha ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi Duniani, OECD, taifa hili lenye uchumi imara kabisa barani Ulaya linawekeza zaidi ya dola bilioni kumi kwenye misaada ya maendeleo.

Sehemu kubwa ya fedha hizi hutoka kupitia bajeti ya Wizara ya Maendeleo, ambayo kwa sasa inafikia euro bilioni 6.4, zinazosaidia miradi kama vile ya ulinzi wa mazingira na hata mikopo kwa serikali. Kwa ujumla, asilimia 0.4 ya uchumi wote wa Ujerumani inatumbukia kwenye misaada, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi tangu kuungana tena kwa Ujerumani, hapo mwaka 1990. Lengo lililowekwa la kufikia asilimia 0.7 ndani ya miaka 20 hii, liko mbali kufikiwa.

Hata kama kinadharia, sehemu ya lengo iliyofikiwa inatoa taswira njema kwa sera ya maendeleo ya Ujerumani, lakini inakosa dhana ya pamoja, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kuwasaidia Watu Wanaokabiliwa na Njaa Duniani, Wolfgang Jamann, ambaye anaona kwamba kuziimarisha taasisi za kiraia katika nchi zinazopokea misaada ndicho kiini cha mafanikio

"Kuna fedha haba sana, mipango michache sana ya muda mrefu. Taasisi za kiraia katika Ghana, India, Cambodia zinahitaji pia msaada kutoka mataifa tajiri ili kuweza kufanya yaliyo muhimu, ambayo ni utawala bora, heshima kwa haki za binaadamu na mengineyo." Amesema Jamann.

Niebel atetea sera ya maendeleo

Mkuu wa Jumuiya ya Weltshungerhilfe, Wolfgang Jamann.

Mkuu wa Jumuiya ya Weltshungerhilfe, Wolfgang Jamann.

Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, anasema ukosoaji huo hauna msingi. Mwanasiasa huyo wa chama cha kiliberali cha FDP, anarejelea masuala kama vile maendeleo ya vijijini na haki za binaadamu ambayo amekuwa akiyasimamia tangu alipochukuwa wadhifa huo miaka miwili na nusu sasa.

Katika mahojiano yake kwa njia ya simu na Deutsche Welle, Niebel amesema madai ya kutolewa kwa fedha kidogo sana "linakera" na badala yake ametetea ushirikiano baina ya Ujerumani na nchi moja moja

"Ukweli ni kwamba, ni jambo lenye maslahi kwa mfadhili kuangalia lile lilo zuri. Ukweli huu ndio unaopelekea matokeo mazuri na ushirikiano wenye ufanisi. Nilikuwa sehemu muhimu ya uanzishwaji wa kile kinachoitwa "mipango ya pamoja" ya Umoja wa Ulaya, ambacho ni ushirikiano wa kimaendeleo kati ya mataifa ya Umoja huo na mataifa yanayopokea sehemu kubwa ya misaada ya wafadhili."

Niebel anasisitiza kwa ushirikiano wa mataifa mengi kwa wakati mmoja unaweza kufanyika tu chini ya taasisi za kifedha za kimataifa, kama vile Benki ya Dunia, kwa sababu unahitaji ufadhili mkubwa wa kifedha.

Sekta binafsi kwenye misaada ya maendeleo

Wakuu wa taasisi za Terre des Hommes na Welthungerhilfe wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Wakuu wa taasisi za Terre des Hommes na Welthungerhilfe wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Lakini wakosoaji wake kwenye taasisi za misaada hawaoneshi kuvutwa na utetezi huu wa Niebel. Katibu Mkuu wa Welthungerhilfe, Jamann, anasema kwamba mawazo ya waziri huyo wa maendeleo ni mazuri kinadharia, lakini si katka utekelezaji, akipigia mfano pale Niebel alipolazimisha kujumuishwa kwa sekta binafsi katika sera ya maendeleo. Jambo ambalo, Jamann anasema, linawanufaisha wachache tu, huku Niebel akisema anashangazwa na namna mashirika ya misaada yanavyoangalia mambo kutokea upande mmoja tu.

Niebel amesema kwamba maendeleo katika mataifa yanayopokea misaada hayapatikani tu kupitia idadi kubwa ya fedha zinazotoka kwa wafadhili, bali zaidi kwa juhudi za ndani za mataifa hayo kupambana na umasikini kwa kutengeneza nafasi mpya za ajira na ukusanyaji wa mapato, ambavyo navyo hatimaye huchochea uwekezaji kwenye sekta za huduma ya jamii, kama afya, elimu na miundombinu.

Kama angelishauriwa yeye, mwenyekiti wa "Terre des Hommes", Danuta Sacher, anasema serikali ya Ujerumani ilipaswa kukusanya fedha zaidi za misaada ya maendeleo kupitia kodi inayotokana na malipo ya fedha, kwani taasisi hizo ndizo chanzo cha kuaminika cha kupatikana kwa kiwango kikubwa cha fedha zinazohitajika. Lakini, angalau kwa hadi sasa, taasisi za kifedha hazijaguswa na dhana nzima ya ushirikiano wa kimaendeleo na serikali inaogopa kuzibinya.

Upinzani mkubwa zaidi umetoka kwa chama cha upinzani cha Die Linke, ambacho msemaji wake masuala ya sera za maendeleo, Heike Hänsel, amesema Waziri Niebel na serikali yake hawajajifunza chochote kutokana na mgogoro wa kifedha.

Mwandishi: Marcel Fürstenau/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Oummilkheir Hamidou

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com