1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal: Faye akaribia ushindi katika uchaguzi wa rais

Bruce Amani
25 Machi 2024

Mgombea wa upinzani nchini Senegal Bassirou Diomaye Faye ameonekana kuongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais ambao ulifanyika baada ya miaka kadhaa ya ghasia na mzozo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/4e4vP
Senegal | mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye
Matokeo ya awali kutoka vituo vya kupigia kura yanamuonesha mgombea wa upinzani Bassirou Faye akiwa kifua mbelePicha: SEYLLOU/AFP

Mshindi wa uchaguzi huo atatwikwa jukumu la kuiongoza Senegal, inayotazamwa kama kinara wa demokrasia katika eneo la Afrika Magharibi lililokumbwa na matukio ya mapinduzi, na kuiondoa katika matatizo yake ya karibuni na kusimamia mapato kutoka kwa hifadhi za mafuta na gesi ambazo zinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni.

Soma pia: Wafahamu wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais Senegal

Sintofahamu ilitanda kuhusu matokeo ya uchaguzi huo, huku matokeo rasmi yakitarajiwa mwishoni mwa wiki na wingi mkubwa wa kura ukihitajika ili kumpata mshindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza.

Uchaguzi wa urais Senegal
Wafuasi wa Faye walisherehekea mitaani Dakar wakati matokeo ya awali yakionesha akiwa kifua mbelePicha: John Wessels/AFP/Getty Images

Kiongozi wa upinzani Faye alikuwa amewaahidi wapiga kura mabadiliko makubwa na ya kweli. Na ameonekana kupata uongozi wa mapema dhidi ya aliyekuwa Waziri mkuu wa zamani wa muungano unaotawala Amadou Ba, kwa mujibu wa matokeo ya awali kutoka vituo vya kupigia kura yaliyochapishwa na vyombo vya Habari vya nchini humo na kwenye mitandao ya kijamii.

Karibu saba kati ya wagombea wa 17 wa urais wamempongeza Faye kutokana na dalili za mwanzo za kura zinazoendelea kuhesabiwa.

"Hongera kwa Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi wake usio na shaka,” mgombea pekee mwanamke, Anta Babacar Ngom, aliandika kwenye mtandao wa X.

Dethie Fall alimpongeza Faye "kwa ushindi wake murwa, uliopatikana hasa kwa kuzingatia mienendo imara inayoibuka”.

Senegal | Rais Macky Sall na Waziri Mkuu Amadou Ba
Amadou Ba (kushoto) wa muungano unaotawala ameelezea matumaini ya kushinda uchaguzi wa raisPicha: SEYLLOU/AFP/Getty Images

Faye, mwenye umri wa miaka 44, na Ba, 62, -- wote wakiwa wakaguzi wa zamani wa ushuru – waliibuka kuwa wagombea waliopigiwa upato kushinda uchaguzihuo kati ya wagombea 17.

Mamia ya watu walikusanyika katika makao makuu ya kampeni ya Faye katika mji mkuu Dakar Jumapili usiku, wakiimba na kucheza ngoma.

Hali ilikuwa ya ukimya zaidi miongoni mwa wafuasi wachache waliokusanyika katika makao makuu ya kampeni ya Ba. Lakini usimamizi wa kampeni yake umesema kwa mujibu wa watalaamu, una "uhakika kuwa, katika hali mbaya zaidi, utakuwa katika duru ya pili”. Ushindi kwa mpinzani Faye huenda ukaanzisha mabadiliko makubwa ya kimfumo nchini Senegal.

AFP