Sebastian Coe kugombea urais wa IAAF
28 Novemba 2014Mshindi mara mbili wa dhahabu katika michezo ya Olimpiki Sebastian Coe amethibitisha kuwa atagombea wadhifa wa rais wa IAAF, wakati Lamine Diack wa Senegal atakapojiuzulu mwaka wa 2015.
Coe amehudumu kama makamu wa rais wa IAAF tangu mwaka wa 2007, na atazindua manifesto yake ya uchaguzi na malengo yake katika mchezo wa riadha na shirikisho linalousimamia katika wiki kadhaa zijazo.
Muingereza huyo mwenye umri wa miaka 58 amesema anataka kuwalenga vijana na uelewa wa kweli wa mazingira ya ulimwengu ambayo yanakikabili kizazi kijacho cha wanariadha na mashabiki. Coe anatarajiwa kukabiliwa na upinzani wa wadhifa wa urais kutoka kwa aliyekuwa bingwa wa Ukraine wa kuruka kwa upondo yaani pole vault Sergey Bubka.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo