Scotland yaweka wazi mipango ya uhuru wa nchi hiyo | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Scotland yaweka wazi mipango ya uhuru wa nchi hiyo

Waziri mkuu wa Scotland ameweka wazi mipango mipya ya kupitishwa kwa kura ya maoni kuhusu uhuru wa Scotland ikiwa maombi yake ya mamlaka zaidi na pia kubaki katika soko la pamoja la umoja wa Ulaya hayatazingatiwa

Nicola Sturgeon ameweka wazi mipango hiyo siku ya alhamis, ambapo alisema kuwa wiki ijayo atachapisha muswada wa kura ya maoni , huku akiishutumu serikali ya Uingereza  kushinikiza kujitoa katika umoja wa Ulaya na kuchochea chuki dhidi ya wageni, kwa mapendekezo yake ya kuweka ukomo kwenye uhuru wa watu kuingia nchini humo.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa bunge la Scotland, Sturgeon amesema mswada wa kura ya uhuru utachapishwa wiki ijayo na kuwasilishwa katika bunge.

Katika kura ya maoni ya mwaka 2014 kuhusu uhuru wa Scotland, wanaopenda kubaki ndani ya muungano wa Uingereza walishinda kwa asilimia 55, lakini Sturgeon amependekeza hali hiyo iangaliwe upya.

"Nimedhamiria kuwa Scotland ifikirie upya kuhusu suala la kujitegemea na kisha kufanya hivyo kabla ya uingereza kujitoa katika umoja wa ulaya, kama hicho ni kitu cha muhimu kwa ajili ya ulinzi wa maslahi ya nchi yetu, na ninathibitisha kuwa muswada wa kujitegemea utachapishwa kwa ajili ya mashauriano wiki ijayo" alisema Sturgeon

Katika kura ya maoni nchini Uingereza kuhusu kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, wascotland wengi walipiga kura kutaka kubaki ndani ya Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Uingereza asema hilo si suala la mjadala kwa sasa

Akizungumzia kauli ya kiongozi huyo, msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amesema kuwa suala hilo lilijadiliwa mwaka 2014, na kuongeza kuwa wanahitaji kuweka msisitizo wa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maslahi ya Uingereza

May kwa upande wake amesema ananuia kukitumia kifungu cha 50 cha mkataba wa Lisbon, kinachoanzisha mchakato wa kujitoa ndani ya Umoja wa Ulaya ifikapo Machi mwaka kesho, kuanzisha mchakato wa miaka miwili wa nchi hiyo kujiondoa kabisa katika Umoja wa Ulaya.  Waziri Mkuu May alisisitiza kuwa mchakato huo wa kujitoa sio suala linaloweza kujadiliwa tena.

"Tulipiga kura kwa pamoja kama nchi moja ya Uingereza,tutajadiliana kama nchi moja ya uingereza na tutaondoka umoja wa Ulaya kama nchi moja" alisema May

Ili kura hiyo ya uhuru wa Scotland iweze kukubalika, Bunge la Uingereza linahitaji kutoa ridhaa. Sturgeon amesema atataka Scotland kubaki katika soko la pamoja la Ulaya, suala tete ambalo kulingana na mawaziri wengi wa Uingereza walionya linaweza kuisababishia Scotland kujiondoa, ikiwa itataka kutatiza udhibiti mkali wa watu wanaoingia nchini Uingereza.  l

Akizungumza na Waziri mkuu May Sturgeon amesema kuwa Scotland haikuchagua kuwa katika hali hiyo isipokuwa ililazimishwa na chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Theresa May.

Nicola Sturgeon amesisitiza kuwa ikiwa Scotland itashindwa, au itakwamishwa kupata maslahi yake ndani ya muungano wa Uingereza, basi itachagua kufuata njia nyingine.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri: Gakuba Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com