Scotland kujaribu kuzuwiya kujitowa kwa Uingereza | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Scotland kujaribu kuzuwiya kujitowa kwa Uingereza

Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon amesema bunge la Edinburgh litajaribu kuzuwiya kujitowa kwa Uingereza Umoja wa Ulaya baada Uingereza yote kupiga kura ya kujitowa na Wascoti kupiga kura ya kuendelea kubakia.

Sturgeon amesema hapo Jumapili (26.06.2016) kwamba "kile kitakachotokea nchini Uingereza ni kwamba kutakuwa na taathira nzito na mbaya ya kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya na nataka kujaribu kuihami Scotland na madahara hayo."

Alipoulizwa atafikiria kuliomba bunge la Scotland kuzuwiya ridhaa yake kwa hatua hiyo ya Uingereza ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC kwamba "Bila ya shaka."

Ameongeza kusema kwamba "Iwapo bunge la Scotland inalipima jambo hilo kwa msingi wa kipi sahihi kwa Scotland hapo tena chaguo la kusema kwamba hatutopiga kura kwa kitu ambacho ni dhidi ya maslahi ya Scotland bila ya shaka hilo litazingawa"

Matamshi hayo mapya ya Strurgeon yanaipa nguvu ahadi aliyoitowa muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura ya maoni ya Alhamisi kuhusu uwanachama wa Uingereza kwa Umoja wa Ulaya.

Amesema "inayumkinika kabisa "kwamba Scotland itataka kuwepo kwa kura ya pili ya maoni kuhusu uhuru wa jimbo hilo kutoka Uingereza kwa sababu matokeo hayo yako kinyume na matakwa ya wapiga kura wa Scotland. Baadae alitaka awe na mazungumzo ya ana kwa ana na maafisa wa Umoja wa Ulaya kujadili uamuzi huo wa Uingereza.

Mgawanyiko wajitokeza

Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon.

Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon.

Wapiga kura wa Uingereza waliamuwa kwa asilimia 52 dhidi ya 48 kujitowa Umoja wa Ulaya wakati Scotland taifa lenye watu milioni tano lilipiga kura ya kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya kwa asilimia 62 dhidi ya 38.

Sturgeon ambaye ni kiongozi wa chama cha National Party chenye kupigania uhuru wa Scotalnd ameonya kwamba taathira za kuiburuza Scotland kutoka Umoja wa Ulaya "dhidi ya matakwa yake" itakuwa na madhara mabaya sana.

Katika mfumo mgumu wa Uingereza wa kugawa baadhi ya madaraka yake ya nchi kwa Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini sheria ilioasisiwa London ya kujitowa rasmi katika Umoja wa Ulaya inabidi ipate ridhaa kutoka mabunge matatu ya majimbo hayo.

Matokeo ya kura hiyo ya maoni yamesababisha fadhaa kubwa nchini Uingereza na duniani kwa jumla. Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na gazeti la Scotland la Sunday Post umegunduwa kwamba asilimia 59 watapiga kura ya kupatiwa uhuru kutoka Uingereza.

Mustakbali wa mashaka

Wanaounga mkono uhuru wa Scotland kutoka Uingereza.

Wanaounga mkono uhuru wa Scotland kutoka Uingereza.

Wachambuzi wa kisheria wameonya kwamba hatua yoyote ile ya Scotland ya kudai uhuru yumkini ikazuiliwa na bunge la Westminster la Uingereza angalau kwa hivi sasa na hata kama itafanikiwa itachukuwa miaka mingi kutekelezwa.

Ombi la Scotland kujiunga na Umoja wa Ulaya linaweza kukwamishwa na nchi nyengine wanachama wa umoja huo kama vile Uhispania ambayo inataka kuepuka hatua kama hiyo ya kudai uhuru kwa jimbo lake la Catalonia.

Lakini kuna mchambuzi mmoja amedokeza kwamba Scotland inaweza kujitangazia uhuru kaba ya hata ya kukamilishwa kwa utaratibu wa kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Hapo inaweza kujieleza kama taifa lenye kurithi nafasi ya uwanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na punguzo la bajeti anasema hayo Andrew Scott profesa wa masomo kuhusu Umoja wa Ulaya katika Chuo Kikuu cha Edinburgh.

Scot anafikiri kwamba Umoja wa Ulaya haina sababu ya kukataa ushiriki au kuendelea uwanachama wa Scotalnd katika Umoja wa Ulaya.

Matokeo ya kura ya maoni yamevitumbukiza chama tawala cha kihafidhina nchini Uingereza na chama cha upinzani cha Labour katika mzozo na pia kuweka alama ya kuuliza juu ya mustakbali wa Ireland ya Kaskazini.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP

Mhariri : Sylvia Mwehozi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com