1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yaomba ushirikiano wa mashabiki

Josephat Charo
10 Desemba 2020

Bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Schalke imeandika barua yenye hisia kali kwa mashabiki Alhamisi (10.12.2020) huku timu hiyo ikiwa na rekodi ya kutoshinda mechi 26 za Bundesliga.

https://p.dw.com/p/3mY1c
Fußball Demonstration von Schalke Fans gegen Clemens Tönnies
Picha: picture-alliance/RHR-FOTO/D. Ewert

"Klabu yetu kwa sasa inajikuta katika hali ambayo hakuna mtu yeyote kati yetu aliyewahi kuishuhudia hapo kabla. Hasa hali uwanjani ni mbaya zaidi kuliko ilivyowahi kutokea kabla," waliandika.

"Ukweli kwamba hatujashinda mchezo wowote kati ya michezo 26 inatia uchungu kwetu sote. Tunajua jinsi mnavyoteseka sana kiasi cha baadhi yenu kuipa kisogo klabu yenu muipendayo katika miezi kadhaa iliyopita."

Katika barua hiyo Schalke inaomba ushirikiano na inaonesha ari ya kufanya mdahalo. "Tunahitaji msaada na mshikamano wenu ambao mara zote umekuwa nembo ya utambulisho wa klabu ya Schalke. Kuwa pamoja ndiyo njia pekee itakayotuwezesha kuendelea kucheza katika ligi kuu ya Bundesliga," inasomeka barua hiyo.

Katika msimu wa sasa wa Bundesliga Schalke wanaburuza mkia katika msimamo wa ligi baada ya kupoteza mara saba na kutoka sare mara tatu katika mechi 10. Wana miadi na Augsburg Jumapili katika jaribio lao lengine la kufikisha mwisho ukame wao wa kutoshinda.

Schalke inapanga kuyajadili masuala yote katika klabu hiyo kwenye mkutano ujao wa wanachama, lakini kutokana na janga la virusi vya corona mkutano huo haujapangiwa tarehe.

(dpa)