Schalke yaingia tena katika msitu wa simba | Michezo | DW | 01.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Schalke yaingia tena katika msitu wa simba

Schalke 04 baada ya kugaragazwa na Real Madrid katikati ya wiki katika mpambano wa Champions League sasa inakabiliwa na kibarua kigumu tena, ambapo inapambana na mshindi asiyeshindika msimu huu Bayern Munich.

Fans in der Bundesliga Schalke 04

Mashabiki wa Schalke uwanjani

Na katika ligi zingine Chelsea ya Uingereza inamatumaini ya kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi ya Uingereza , wakati Ronaldo anarejea katika ligi ya Uhispania, La Liga baada ya kutumikia adhabu ya kutocheza michezo mitano.

Wakiwa bado wanauguza vidonda baada ya kubugizwa mabao 6-1 na Real Madrid ya Uhispania , Schalke 04 inaingia katika mtihani mwingine mgumu jioni ya leo wakati watakapokuwa wageni wa Bayern Munich ambayo haijapoteza mchezo msimu huu.

Bundesliga Schalke Leverkusen Julian Draxler

Julian Draxler

Hakuna cha kuhofia

Hatuna uchaguzi , ila kuachana na hisia za mchezo huo, amesema mchezaji wa kati wa Schalke Julian Draxler baada ya kimbunga kilichowakuta dhidi ya Real Madrid.

Tunapaswa kuondoa kichwani mwetu mchezo huo na kujitayarisha dhidi ya Bayern.

Fußball DFB-Pokal Viertelfinale Eintracht Frankfurt - Borussia Dortmund

Wachezaji wa Borussia Dortmund

Schalke inakabiliwa na mlima mwingine mkubwa na changamoto kubwa zaidi dhidi ya Bayern , timu ambayo imeshinda michezo yake yote 14 na wameweka rekodi sasa ya kushinda michezo 47 bila kufungwa.

Bayern ni wazuri zaidi ya Real Madrid, lakini hatuendi kwao kupunguza madhara, amesema mkurugenzi wa spoti wa Schalke Horst Heldt.

Ushindi wa mabao wa 4-0 wa Bayern dhidi ya Hannover 96 wiki iliyopita umekiweka kikosi hicho cha Pep Guardiola mabingwa wa Ulaya points 19 mbele katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga .

Nyota wa Bayern Bastian Schweinsteiger anatarajiwa kuwamo tena katika kikosi cha kwanza kwa mara ya pili baada ya kurejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Borussia Dortmund ambayo inashikilia nafasi ya tatu katika Bundesliga inaikaribisha Nuremburg leo jioni bila hakika ya kuwa na mlinzi wao Socrates ambaye ni majeruhi.

DFB Joachim Löw Trainer

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew

Bayer Leverkusen inayoshikilia nafasi ya pili , inaikaribisha Mainz 05 , huku ikikabiliwa pia na kuporomoka katika kujiamini baada ya vipigo vya kutisha hivi karibuni mara saba katika michezo tisa.

Michezo mingine jioni ya leo(01.03.2024) ni kati ya Werder Bremen ikipambana nyumbani dhidi ya Hamburg SV, Augsburg inaikaribisha Hannover 96, na Eintracht Braunschweig ina miadi na Borussia Moenchengladbach.

Naye kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amemteua mchezaji wa kati Bastian Schweinsteiger kurejea katika kikosi cha timu ya taifa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Chile siku ya jumatano wiki ijayo baada ya kupona kifundo cha mguu, ambapo pia kocha huyo amewaita kikosini wachezaji wengine wanne wapya.

Schweinsteiger , ambaye alicheza mchezo wake wa 100 dhidi ya Sweden Oktoba mwaka jana anaungana pia na mchezaji wa kati wa Borussia Dortmund Kevin Grosskreuz, ambaye aliwahi kuwamo kundini Februari mwaka 2011.

Wachezaji chipukizi walioteuliwa ni pamoja na Matthias Ginter wa Freiburg na Shkodran Mustafi wa Sampdoria pamoja na mshambuliaji wa Hamburg SV Pierre-Michel Lasogga na mchezaji wa kati wa Augsburg Andre Hahn.

Premier League

Katika ligi ya Uingereza, Premier League mlinzi wa Chelsea Gary Cahill amekiri kuwa timu hiyo ina fursa ya kuchukua hatua moja zaidi kuelekea katika ubingwa wa ligi hiyo wakati itakapokumbana na Fulham leo jioni.

Champions League - FC Schalke 04 gegen Chelsea

Mlinzi wa Chelsea Ivanovic akishangiria bao

Wakati huo huo Brendan Rodgers anaamini kuwa Liverpool itakuwa mpizani tofauti kabisa na timu iliyoshindwa na Southampton mapema katika msimu huu wakati kikosi hicho kikijitayarisha kwa ziara muhimu katika uwanja wa St Mary leo jioni kupambana na Southampton.

Katika michezo mingine Arsenal London wako ugenini kupambana na Stoke City , Everton iko nyumbani ikiisubiri West Ham United , na Hull City ina miadi na Newcastle.

Real Madrid inaingia uwanjani kuumana katika mchezo wa nne wa watani wa jadi msimu huu dhidi ya Atletico Madrid kesho Jumapili na kikosi hicho kitaongezewa nguvu na kurejea kwa Cristiano Ronaldo ambaye amemaliza adhabu yake ya kutocheza michezo mitano.

Barcelona itajitupa dimbani pia kesho Jumapili (02.03.2014) ikiikaribisha nyumbani Almeria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Josephat Charo