1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SC Paderborn yakaribishwa katika Bundesliga

12 Mei 2014

Bayern Munich huenda walisherehekea taji lao la 24 la Bundesliga wikendi hii, nao makocha Thomas Tuchel na Huub Stevens wakaziaga klabu zao, lakini hadithi kuu inaihusu klabu ya SC Paderborn 07

https://p.dw.com/p/1ByP5
Fußball 2. Bundesliga 34. Spieltag SC Paderborn 07 gegen VfR Aalen
Picha: picture-alliance/dpa

Timu hiyo ya daraja ya pili ya Bundesliga, ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo, na kuinyima Greuther Fürth nafasi ya mwisho ya moja kwa moja ya kupandishwa ngazi. Hii ni baada ya Paderborn kuwazaba VfR Aalen magoli mawili kwa moja. Mario Vrancic ndiye aliifungia Paderborn goli la kwanza

Greuther Fürth sasa watapambana na SV Hamburg katika mechi ya mchujo wiki ijayo kuamua ni nani atajiunga na Fc Köln na Paderborn katika ligi kuu ya soka Ujerumani. Klabu hiyo ndogo kila mara imekuwa ikicheza katika kivuli cha miamba na mahasimu wao Borussia Dortmund na hata Arminia Bielefield lakini sasa mambo yamebadilika.

Katika habari nyingine za Bundesliga, kocha wa Mainz 05 Thomas Tuchel amejiuzulu jana baada ya kuongoza kwa miaka mitano, na baada ya klabu hiyo kufuzu katika nafasi ya kucheza Europa League msimu ujao. Tuchel aliifahamisha timu kuhusu uamuzi wa kuondoka kwake baada ya ushindi wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya Hamburg SV ambao uliwaweka katika nafasi ya saba msimu huu na nafasi ya kucheza mechi ya mchujo kujitakia tikiti ya Europa League. Kocha mwingine aliyeamua kusalimu amri ni Mholanzi Huub Stevens ambaye ameiaga klabu ya Stuttgart, baada ya kufaulu katika juhudi zake za kuwaepusha mabingwa hao wa Bundesliga mwaka wa 2007 dhidi ya fedheha ya kushushwa daraja.

Hamburg sasa watapambana na Fürth ili kuamua hatima yao katika Bundesliga
Hamburg sasa watapambana na Fürth katika mechi ya mchujo ili kuamua hatima yao katika BundesligaPicha: Getty Images

Stevens mwenye umri wa miaka 60 alisema anaondoka kwa sababu za kibinafsi, na sasa anachohitaji tu ni likizo. Stuttgart ilimaliza msimu katika nafasi ya nne kutoka nyuma, baada ya kufungwa goli moja kwa sifuri na Bayern katika siku ya mwisho ya msimu.

Kabla ya siku ya mwisho ya msimu, haikujulikani ninani angepewa tuzo ya mfungaji bora wa msimu, kati ya Mario Mandzukic na Robert Lewandowski. Lakini baadaye ilibainika kuwa mshindi wa tuzo hiyo ni lewandoswki ambaye magoli yake mawili aliyoifungia Borussia Dortmund yalimpa ushindi dhidi ya mchezaji mwezake atakayechukua nafasi yake msimu ujao Mandzukic. Alimaliza msimu kwa kufunga magoli 20 mawili zaidi dhidi ya Mandzukic. BvB waliwazaba Hertha Berlin magoli manne kwa sifuri.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman