SADC yatakiwa kuzungumzia ukiukaji wa haki za binaadamu | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

SADC yatakiwa kuzungumzia ukiukaji wa haki za binaadamu

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika-SADC, imetakiwa kuzungumzia na kushughulikia ukiukwaji wa haki za binaadamu miongoni mwa nchi wanachama, kama sehemu ya kuimarisha ustawi wa watu wake

Rais Robert Mugabe, mwenyekiti ajaye wa SADC

Rais Robert Mugabe, mwenyekiti ajaye wa SADC

Wito huo umetolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu mjini Hahare, Zimbabwe. Katika ripoti ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya Mawakili wa Haki za Binadamu nchini Zimbabwe, Amnesty International pamoja na Human Rights Watch, zimeelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na rekodi mbaya ya haki za binaadamu nchini Angola, Malawi, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.

Ripoti hiyo imetolewa jana, wakati ambapo nchi wanachama 15 wa SADC, wakijiandaa na mkutano wa kilele wa 34 utakaowajumuisha wakuu wa serikali, utakaofanyika tarehe 17 na 18 ya mwezi huu mjini Harare.

Mashirika hayo yameelezea wasiwasi wao mkubwa kutokana na rekodi mbaya ya haki za binaadamu kwenye nchi hizo, ikiwemo Zimbabwe, ambayo itachukua uenyekiti wa SADC.

SADC imekuwa ikikosolewa kutokana na kusita kuzichukulia hatua nchi wanachama wake kutokana na kuikuka haki za binaadamu.

Zimbabwe yashindwa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa

Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch, Kenneth Roth

Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch, Kenneth Roth

Mkurugenzi wa Mawakili wa Haki za Binadamu nchini Zimbabwe, Irene Petras, ameishutumu Zimbabwe kwa kushindwa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa machafuko ya kisiasa katika chaguzi zilizopita pamoja na kulaani usiri unaozunguka haki za uchimbaji madini na faida kubwa zinazotokana na viwanja vya almasi nchini humo.

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Kusini mwa Afrika, Deprose Muchena, amesema haki za binaadamu ni sehemu kubwa ya kufikiwa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda.

Amesema SADC wanapaswa kujitahidi kujenga mazingira kwa watu wote kufurahia haki zao za kiuchumi, kijamii, kiraia na kisiasa.

Mashirika hayo yanasema uongozi wa SADC unapaswa kutekeleza mahitaji ya watu wa kawaida na kutekeleza viwango vya haki za binaadamu kikanda na kimataifa.

Chini ya uongozi wa Zimbabwe, SADC inalazimika kushinikiza kuimarishwa kwa haki za binaadamu katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara, hasa Angola, Malawi, Swaziland na Zambia.

Ripoti za ukiuakaji haki za binaadamu zazuiwa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Angola na Swaziland kila mara huwakandamiza waandamanaji na watu wanaoikosoa serikali na hata kuzuia ripoti za vyombo vya habari kuhusu ukiukaji wa haki za binaadamu.

Ingawa katiba ya Angola ya mwaka 2010 inahakikisha ulinzi wa kimataifa wa haki ya uhuru wa kujieleza na mikutano ya amani pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, serikali imezidi kukandamiza haki hizo.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty

Haki za binaadamu zimekuwa zikizidi kukiukwa nchini Zambia tangu Rais Michael Sata alipoingia madarakani mwaka 2011. Taifa hilo limetumia vibaya sheria kuwatesa wanachama wa upinzani pamoja na mashoga.

Ripoti hiyo imesema ni lazima Malawi iingize haki za binaadamu za kimataifa katika sheria yake ya taifa na iwalinde mashoga. Hata hivyo, uchaguzi wa mwezi Mei nchini Malawi, ulionyesha nguvu na uhuru wa taasisi muhimu za serikali, ikiwemo mahakama, vikosi vya usalama na chombo cha kusimamia uchaguzi.

Tiseke Kasambala, Mkurugenzi wa Human Rights Watch Kusini mwa Afrika anasema ili kufanikisha mada ya mkutano wa kilele wa SADC ya ''Mabadiliko ya Kiuchumi'', Zimbabwe na nchi nyingine za kanda hiyo, zinapaswa kuimarisha na kukuza utawala bora, kutekeleza utawala wa sheria na kuheshimu haki za binaadamu. Kasambala anasema uwazi halisi na haki, zitasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi ya SADC na hivyo kuimarisha maisha ya watu wake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,HRW Press
Mhariri:Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com