Ruto aitisha kikao maalum kujadili athari za mafuriko
30 Aprili 2024Ruto alisema kikao hicho kilitarajiwa kujadili juu ya hatua za ziada katika kushughulikia mzozo huo na kuongeza kuwa lazima serikali iwaangalie wananchi ambao ni waathirika wa mabadiliko ya hali ya hewa.
Viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na watetezi wa haki za binadamu nchini humo wameishutumu serikali ya Ruto kwa kutokufanya ya kutosha, licha ya tahadhari iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa na kuitaka itangaze mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa.
Soma zaidi: Rais Ruto atangaza mikakati ya kukabiliana na mafuriko
Mvua kubwa kuliko kawaida ikichangiwa na hali ya El Nino imeshuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwemo miundombinu ya barabara, kughariki kwa vijiji na kutishia uharibifu zaidi katika siku za usoni.
Katika mkasa mbaya zaidi hadi sasa, siku ya Jumatatu (Aprili 29), kingo za Bwawa la Kijabe zilipasuka na kusababisha vifo vya takribani watu 50.