RENAMO wavunja mkataba wa amani Msumbiji | Matukio ya Afrika | DW | 22.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

RENAMO wavunja mkataba wa amani Msumbiji

Chama cha upinzani nchini Msumbiji Renamo kimejiondoa katika mkataba wa amani kilioutia saini mwaka wa 1992 na chama tawala cha Frelimo ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Hatua hiyo imezusha hofu ya kuanza tena mgogoro katika nchi hiyo ya Afrika inayoinukia kama mojawapo ya nchi zinazotengeneza nishati. Chama cha Renamo kiliingia katika siasa za uwakilishi kupitia muafaka wa amani ambao ulimaliza vita vya mwaka wa 1975-1992, kimesema kimechukua uamuzi huo kufuatia hatua ya jana Jumatatu ya majeshi ya serikali kuiteka kambi moja ya msituni ambayo kiongozi wake Afonso Dhlakama alikuwa akiishi. Dhlakama alitoroka na kujificha katika milima iliyo karibu na msitu huo.

Msemaji wa Renamo Fernando Mazanga amesema “amani imekwisha nchini humo….na sasa ni jukumu la serikali ya Frelimo kwa sababu haikutaka kusikia malalamiko ya Renamo”. Mazanga amesema chama cha Renamo, ambacho kina wabunge 51 katika bunge la sasa lenye wabunge wengi wa Frelimo, kitaandaa mkutano ili kuamua mkakati wake. Hajasema maramoja kama kundi hilo la upinzani litachukua tena silaha katika kiwango cha kitaifa.

Vita vya Msumbuji vilivyodumu miaka 16 vilisababisha vifo vya takribani watu laki sita

Vita vya Msumbuji vilivyodumu miaka 16 vilisababisha vifo vya takribani watu laki sita

Hapajakuwa na tamko la haraka kutoka upande wa serikali ya Rais Armando Emilio Guebuza. Awali, ilithibitisha kuwa wanajeshi wake wametwaa kambi ya Renamo katika eneo la Gorongosa la mkoa wa Sofala, karibu kilomita 600 kaskazini ya mji mkuu Maputo. Hayo yalifuatia makabiliano katika sehemu hiyo baina ya jeshi na Renamo.

Uamuzi wa moja kwa moja wa kuuvunja mkataba huo bila shaka utazitahadharisha serikali za wafadhili na wawekezaji, ambazo zimekuwa zikisaidia maendeleo ya kiuchumi nchini Msumbiji ambayo ni mojawapo ya nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi barani Afrika. Mapigano hayo ndani ya msitu wa Gorongosa baina ya pande hizo mbili hasimu yametokea mwezi mmoja tu kabla ya kuandaliwa uchaguzi wa manispaa ambao Renamo iliahidi kususia na kuuvuruga kwa sababu inakishutumu chama cha Frelimo kwa kuendeela kusalia madarakani.

Serikali ya Guebuza nayo inakishutumu chama cha Renamo kwa kujaribu kuidhoofisha Msumbiji na kuirudisha tena katika vita. Jeshi la Msumbuji liliivamia kambi ya Dhlakama baada ya watu wanoshukiwa kuwa wapiganaji wa Renamo kuwauwa wanajeshi saba wa serikali katika shambulizi la wiki iliyopita. Mashambulizi ya Renamo ya mwezi Aprili na Juni katika eneo la Sofala tyari yalikuwa yamezusha hofu ya uimara wa Msumbiji. Waliwauwa karibu wanajeshi 11 na polisi, pamoja na raia sita na kulazimisha kusitishwa kwa muda mauzo ya makaa ya mawe yanayosafirishwa kwa njia ya reli kuelekea pwani. Usafiri wa barabarani pamoja na biashara ya watalii pia viliathirika.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Josephat Charo