1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid yaifurusha Chelsea katika Ligi ya Mabingwa

Daniel Gakuba
19 Aprili 2023

Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wametinga nusu fainali baada ya kuibugiza Chelsea magoli mawili kwa sufuri kwenye uwanja wa Stamford Bridge mjini London

https://p.dw.com/p/4QHXj
Champions League Chelsea and Real Madrid Rodrygo
Picha: Adrian Dennis/AFP

Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wametinga nusu fainali baada ya kuibugiza Chelsea magoli mawili kwa sufuri kwenye uwanja wa Stamford Bridge mjini London, na ukiongeza mengine 2-0 kutoka mechi ya kwanza mjini Madrid wiki iliyopita, Chelsea inayaanga mashindano kwa kichapo cha nne bila jibu.

Soma pia: Mabingwa watetezi Real Madrid waishinda Chelsea 2-0

Magoli yote mawili ya Real Madrid yamepachikwa kimiani na Rodrygo, la kwanza mnamo dakika ya 58 ya mchezo, na na la pili lililozamisha kabisa matumaini yoyote ya Chelsea kuambulia chochote likasukumizwa wavuni kwenye dakika ya 80 ya mchezo.

Chelsea walianza vizuri mchezo na kiungo wao Ngolo Kante mara mbili alikosakosa kuzitingisha nyavu, na kipa wa Real Madrid Thibaut Courtois alifanya kazi ya ziada kuizuia klabu yake ya zamani kwenda mapumziko ikiwa na mtaji wowote wa magoli.

Milan yaizidi nguvu Napoli

Fußball Champions League | SSC Neapel - AC Mailand
Milan walifuzu licha ya sare ya 1-1 mjini NaplesPicha: Andrea Staccioli/Insidefoto/IMAGO

Katika mechi nyingine ya robo fainali usiku wa kuamkia leo, AC Milan ilisalimika mbele ya shinikizo la Napoli na kufuzu ngazi ya nusu fainali kwa kuponyoka na ushindi wa magoli mawili kwa moja kutoka mechi mbili.

Alikuwa Olivier Giroud wa AC Milan aliyeliona lango kwanza dakika chache kabla ya kwenda mapumziko ya nusu ngwe, na jitihada za kufa na kupona za Napoli hazikuzaa matunda hadi katika kipindi cha nyongeza, pale Victor Osimhen alipozawazisha na kumaliza mechi ya jana kwa sare ya goli 1-1.

AC Milan ambayo ushindi wake wa goli 1-0 katika mechi ya awali umeisadia kukata tiketi ya nusu fainali, inasubiri kujua mpanzani wake baadaye leo, kati ya Inter Milan na Benfica.

Macho ya mashabiki wengi yataelekezwa huko Allianz Arena mjini Munich kuona kama mabingwa hao wa Ujerumani watajinasua mbele ya Manchester City, inayosafiri kuja Ujerumani ikiwa na akiba ya magoli 3 kibindoni. Bruce Amani anaeleza matarajio yake katika mechi mechi hizo mbili za baadaye leo usiku, hasa kiunzi kirefu mbele ya Bayern.

Baada ya mechi za leo usiku itajulikana nani kati ya Manchester City na Bayern Munich atakabiliana na Real Madrid, na japo mpira unadunda, atakayevuka ngazi ya nusu fainali kati ya miamba hiyo ya soka, atapigiwa upatu kuutwa ubingwa.

AFP, Reuters, DPA, AP