Ravalomanana ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ravalomanana ajiuzulu

Kishindo cha Rajoelina na wafuasi wake cha mng'owa madarakani rais wa kisiwa cha Madagascar

default

Rais Marc Ravalomanana ayapa kisogo madaraka yake

Rais Marc Ravalomanana wa Madagascar amejiuzulu na kumkabidhi hatamu za uongozi  admeri Hypolite Ramaroson, kufutia miezi miwili ya mzozo ulioshadidiwa na miito na onyo la upande wa upinzani na jeshi.Hapo awali mkuu wa upande wa upinzani wa Madagascar, Andry Rajoelina, akiongozana na umati wa mashabiki wake, waliingia kifua mbele katika kasri la rais kati kati ya mji mkuu, Antananarivo,kasri lililovamiwa jana usiku na jeshi kwa lengo la kuharakisha kung'atuka madarakani rais Ravalomanana.


"Ninaahidi nitafanya kila niwezalo.Tuko huru sasa lakini njia bado ni ndefu na ngumu."alisema kiongozi huyo wa upande wa upinzani mwenye umri wa miaka 34.


Marc Ravalomanana,mfanyabiashara tajiri aliyeingia madarakani kwa sauti za umma mnamo mwaka 2002 ametia saini "hati " akimkabidhi hatamu za uongozi tangu wake yeye binafsi mpaka  uongozi wa waziri mkuu,afisa aliyetumikia jeshi kwa muda mrefu zaidi,admirali Hypolite Ramarason.


Ufafanuzi wa hati hiyo haujulikani na haijulikani pia wapi amekimbilia rais huyo aliyejiuzulu.


Siku za hivi karibuni wadadisi wengi walikua wakiashiria uwezekano wa Ravalomanana kukimbilia uhamishoni,kutokana na ile hali kwamba familia yake yote imeshakihama kisiwa hicho cha bahari ya Hindi.


Leo asubuhi Marc Ravalomanana alisisitiza "yuko tayari kufa kuliko kuachana na haki yake".


Mzozo kisiwani Madagascar umeripuka Disemba mwaka jana baada ya serikali kukifunga kituo cha televisheni kinachomilikiwa na upande wa upinzani.


Andry Rajoelina, aliyeunda serikali mbadala tangu siku kadhaa zilizopita, alipokea hapo awali hati za mawaziri kadhaa waliompa kisogo Ravalomanana.


Mwishoni mwa wiki, jeshi ambalo kawaida halielemei upande wowote, liliamua kumuunga mkono meya huyo wa zamani wa mji mkuu ambae wafuasi wake walikusanyika tangu asubuhi wakihanikiza kwa makelele kumsifu kiongozi wao.


Katika wakati ambapo Umoja wa Afrika, AU, umetoa mwito Rajoelina asikabidhiwe hatamu za uongozi, jeshi la Madagascar linasema yeye ndie anaebidi kuiongoza nchi hiyo.


Andry Rajoelina ambae ameshakabidhiwaa funguo za majengo yote ya rais, ameahidi kutunga katiba mpya na kuitisha uchaguzi wa rais na wa bunge mnamo mwaka ujao.


Hapo awali Umoja wa Ulaya ulitishia kusitisha msaada wake kwa Madagascar pindi rais mpya akiingia madarakani kwa msaada wa kijeshi.


Muandishi;Hamidou Oummilkheir /AFP/ Reuters

Mhariri:Othman MIraji
 • Tarehe 17.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HEDh
 • Tarehe 17.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HEDh
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com