1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rashford alalamikia ubaguzi wa rangi

Lilian Mtono
27 Mei 2021

Marcus Rashford amesema ametupiwa kejeli za ubaguzi wa rangi kupitia kwenye mitandao ya kijamii baada ya kikosi chake cha Manchester United kuondolewa kwenye fainali ya michuano ya Ligi ya Europa.

https://p.dw.com/p/3u35T
Manchester United v RB Leipzig I Marcus Rashford
Picha: Anthony Devlin/AFP/Getty Images

Marcus Rashford amesema amejikuta katika wakati mgumu baada ya kutupiwa kejeli za ubaguzi wa rangi kupitia kwenye mitandao ya kijamii baada ya kikosi chake cha Manchester United kuondolewa kwenye fainali ya michuano ya Ligi ya Europa.

Rashford 23 ambaye tayari amekuwa muhanga wa mashambulizi hayo ya ubaguzi wa rangi amesema ametupiwa angalau vijembe 70 vya kibaguzi baada ya kupoteza mkwaju wa penati wakati walipokwaana na Villareal katika fainali hizo huko Gdansk jana Jumatano

Baada ya kushindwa kwa penati 11-10 Manchester United baadae iliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba wachezaji wake walikabiliwa na jumbe mbaya na za ubaguzi wa rangi.

"Nilikasirishwa sana na mtu mmoja aliyenitumia ujumbe wenye picha ya nyani, na huyo ni mwalimu wa hesabu. Anawafundisha watoto!! Na anajua kwamba anaweza kuwabagua watoto bila ya kukabiliwa na hatua yoyote..." 

Mwezi uliopita shirikisho la soka la England pamoja na taasisi nyingine za michezo ziliungana pamoja kwa siku nne kususia mitandao ya kijamii kwa kuyataka makampuni kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alipozungumza kabla ya tukio hili la karibuni, kocha wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate alisifu juhudi za wachezaji katika kupambana na matukio ya ubaguzi wa rangi.

Katika kipindi cha miezi 12 sasa wachezaji wamekuwa wakipaza sauti zao kukemea vitendo hivyo vya ubaguzi wa rangi.

Mashrika: AFPE