1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Afrika ya Kati atangaza kura ya maoni ya katiba

31 Mei 2023

Rais Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza kura ya maoni kwa ajili kupata katiba mpya, ambayo wapinzani wake wanasema ni mbinu ya kumruhusu kuwania tena muhula mwengine madarakani.

https://p.dw.com/p/4S0Uw
CENTRAL AFRICAN REPUBLIC-BANGUI-ELECTIONS-CAMPAIGN
Picha: Andr.B/Xinhua News Agency/picture alliance

Bila ya kutaja tarehe rasmi ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni, Rais Touadera alitangaza utetezi na azma yake ya kuitisha kura hiyo kupitia hotuba iliyorushwa moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa Facebook, akisema hawezi kupuuzia matakwa ya umma.

"Nikiwa rais niliyechaguliwa kidemokrasia, siwezi kupuuzia matakwa halali ya wananchi ya kuipatia nchi yetu katiba mpya. Uratibu wa kura ya maoni chini ya masharti ya Katiba hauwezi kuonekana kuwa ni njia ya rais wa jamhuri kuzuwia mabadiliko ya kisiasa, hakikisho la demokrasia na utawala wa sheria," alisema.

Soma zaidi: Guterres awakosoa walinda usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wapinzani wa rais huyo aliyeingia madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka 2016 na kurejea tena mwaka 2020 wanamtuhumu kwamba anataka kutumia mabadiliko ya katiba kuondosha ukomo wa kuwapo madarakani. 

Mnamo mwezi Januari, Rais Touadera alimuondosha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba, Daniele Darlan, baada ya jaji huyo kupingana na kile alichokiita "mapinduzi kwa jina la katiba" akizungumzia amri ya rais kufanya mapitio ya katiba. 

Kwa mujibu wa katiba ya sasa, rais anaweza kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka minne minne tu madarakani.

Kuelekea urais wa maisha?

"Hakutakuwa na muhula wa tatu, lakini mabadiliko haya yatarejesha kila kitu mwanzo kabisa. Kwa hivyo mtu yeyote anaweza kuwania urais, akiwemo Touadera kama atataka." Alisema mshauri mkuu wa Touadare kwenye masuala ya siasa, Fidele Gouandjika, alpozungumza shirika la habari la AFP.

Bangui I Wahlen in Zentralafrika
Upigaji kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.Picha: AP/picture alliance

Waziri mkuu wa zamani, Nicolas Tiangaye, amesema katiba mpya inayopendekezwa na Touadare ina azma ya kumgeuza kiongozi huyo kuwa rais wa maisha.

Soma zaidi: Uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakabiliwa na vurugu

Tiangaye, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa upinzani, amesema hatua hiyo ni kinyume na katiba kwa kuwa Mahakama ya Katiba iliyopo sasa "haina uhalali wa kisheria tangu kuondolewa kwa Jaji Mkuu Darlan."

Kando na hayo, Touadera anakosolewa vikali kwa kukodi wapiganaji wa kundi la Wagner kutoka Urusi kukabiliana na wanamgambo wanaohodhi sehemu kubwa ya nchi yenye utajiri wa madini na rasilimali nyenginezo. 

Kabla ya hapo, Ufaransa ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya wanajeshi wake kwenye koloni lake hilo la zamani, lakini ililazimika kuwaondosha kufuatia mgogoro wa kisiasa baina ya Paris na Bangui.

Chanzo: AFP
Mhariri: Daniel Gakuba