1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bashir akabidhi uongozi wa chama kwa makamu wake

Sylvia Mwehozi
1 Machi 2019

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir amekabidhi uongozi wa chama tawala nchini humo kwa makamu wake aliyeteuliwa hivi karibuni, mnamo jumla ya waandamanaji wanane wanaoipinga serikali wakihukumiwa kifungo jela Alhamis jioni. 

https://p.dw.com/p/3EIJ1
Sudan Omar al-Bashir ARCHIV
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Bashir amemkabidhi uongozi Ahmed Harun kama kaimu mwenyekiti wa chama cha NCP hadi mkutano mkuu ujao wa chama utakapofanyika na rais mpya wa chama kuchaguliwa. Bashir alimteua Harun kama mwenyekiti msaidizi wa NCP, wakati alipofanya mabadiliko makubwa kwenye serikali yake kwa lengo la kukabiliana na maandamano yanayoendelea.

Hata hivyo makamu huyo mpya anatakiwa na mahakama ya jinai ya ICC iliyoko mjini the Hague kwa makosa ya uhalifu wa kivita mjini Darfur, kama ilivyo kwa rais Bashir mwenyewe. Chama cha NCP kina wingi wa viti bungeni na kwa mujibu wa kanuni zake, mkuu wa chama ndiye anakuwa na nafasi ya kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais, uliopangwa kufanyika mwaka 2020.

Wakati huo huo, waandamanaji wanane wanaoipinga serikali wamehukumiwa kifungo cha jela jana jioni. Adhabu hiyo ni ya kwanza kutolewa na mahakama maalum ya dharura iliyoanzishwa na Rais Bashir ili kupambana na watu wanaomtaka ajiuzulu.

Sudan | Protest
Waandamanaji wanaomshinikiza rais Bashir ajiuzuluPicha: Reuters/M. N. Abdallah

Waandamanaji hao wanane walikuwa ni miongoni mwa mamia waliomiminika mitaani mapema siku ya Alhamis mjini Khartoum na Omdurman, wakikiuka marufuku ya kufanya maandamano yaliyoanza kwa mara ya kwanza mwezi Desemba juu ya kupanda gharama za maisha na tangu wakati huyo yakapamba moto na kutoa shinikizo kubwa kwa utawala wa miongo mitatu wa Bashir.Waziri mkuu Mohamed Tahir Ayala aliyeapishwa hivi karibuni amesema kuna jitihada za kushughulikia changamoto zilizopo.

"Nimejadiliana na rais kuhusu kazi inayotakiwa kufanyika na mazungumzo na vyama vyote vya siasa juu ya kuwa na mpangilio ambao utaweza kuanzisha serikali fanisi na iliyo na uwezo wa kushughulikia masuala ya kitaifa na kutimiza matakwa ya na matamanio ya watu," alisema waziri mkuu. 

Bashir sio tu amepiga marufuku mikutano bali pia amekabidhi mamlaka kwa vikosi vya usalama kufanya uvamizi na upekuzi binafsi kama sehemu ya hali ya dharura ya nchi nzima iliyotangazwa baada ya jaribio la kukabiliana na maandamano kushindwa.

Waandamanaji hao wanane wamehukumiwa kifungo jela cha kati ya miezi sita hadi miaka mitano na mahakama tatu tofauti mjini Khartoum. Kwenye taarifa yake muungano wa mawakili wa demokrasia ambao ni sehemu ya kundi linaloongoza harakati dhidi ya utawala wa Bashir umesema kuwa kiasi ya waandamanaji 870 walifikishwa mahakamani mjini Khartoum katika kipindi hicho cha hali ya dharura na katika mji pacha wa Omdurman siku ya Alhamis. Mamlaka zinasema jumla ya watu 31 wameuawa katika vurugu zinazohusiana na maandamano hadi hivi sasa lakini shirika la Human Rights Watch linasema jumla ya watu 51 wameuawa.