Raia wa Jamhuri ya Congo wataka katiba ibadilishwe | Matukio ya Afrika | DW | 27.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Raia wa Jamhuri ya Congo wataka katiba ibadilishwe

Asilimia 92 ya wapiga kura wa Congo wameridhia mabadiliko ya katiba yatakayomruhusu rais Nguesso kugombea muhula wa tatu. Hii ni kulingana na kura ya maoni iliopigwa nchini humo siku ya Jumapili.

Kulingana na matokeo ya kura hiyo ya maoni yaliotangazwa rasmi, wapiga kura wamekubali rais huyo kurefusha kipindi chake cha miaka 31 madarakani. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Raymond Mboulou amesema asilimia 92.96 ya wapiga kura tayari wameidhinisha mabadiliko ya katiba, ambayo yameanza kutekelezwa.

Hata hivyo, matokeo rasmi yanaonyesha asilimia 72.44 ya wananchi walishiriki katika kura hiyo, ijapokuwa hapo Jumatatu kiongozi wa upinzani Pascal Tsaty Mabiala alisema ni asilimia 10 tu ndio iliyojitokeza kupiga kura. Upinzani ulisusia kura hiyo na kutaka ifutiliwe mbali kutokana na idadi hiyo kuwa ndogo.

Upinzani umesema tangazo la tume kwamba asilimia 72 ya watu walijitokeza kupiga kura ni habari ya uwongo, na kuyataja matokeo hayo kuwa ya udanganyifu. Clement Mierassa kiongozi wa chama cha upinzani cha Social Democratic amesema matokeo hayo yanayonesha nia mbaya na udanganyifu mkubwa uliofanyika kuyachakachua.

Mgombea hatakiwi kuwa na zaidi ya miaka 70

Brazaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo

Brazaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo

Aidha taarifa nyengine zinasema kulikuwa na mlolongo mkubwa wa wapiga kura karibu na ikulu ya rais Denis Sassou Nguesso, mahali ambapo, Nguesso mmoja wa marais waliokaa muda mrefu madarakani barani Afrika alipopiga kura yake. Kwa upande wake tume ya uchaguzi nchini humo imesema zaidi ya watu milioni 1.2 walipiga kura wakitaka mabadiliko ya katiba huku watu takriban 102,000 wakipinga.

Kura hiyo ya maoni ilipendekeza mabadiliko mawili katika katiba hiyo ambayo kwa sasa inamyima Sassou Nguesso nafasi ya kugombea tena urais mwaka 2016, kwa sababu inaeleza wazi kwamba mgombea wa urais hatakiwi kuzidi umri wa miaka 70 na kuweka kikomo cha vipindi viwili tu kwa rais kuiongoza nchi hiyo. Kwa sasa rais Nguesso amepindukia miaka hiyo na tayari ameshaitumikia nchi hiyo inayozalisha mafuta kwa wingi mihula miwili ya miaka saba kila mmoja

Rais Denis Sassou Nguesso aliiongoza Congo Brazzaville kuanzia mwaka wa 1979 hadi mwaka wa 1992, aliposhindwa katika uchaguzi wa urais. Utawala wake ukarejea tena miaka mitano baadaye baada ya vikosi vyake vilivyoshinda vikosi vya rais wa wakati huo katika vita vya muda mfupi vya wenyewe kwa wenyewe.

Nguesso ni rais wa hivi karibuni barani Afrika anayejaribu kurefusha muda wake madarakani kwa kubadilisha katiba. Hatua kadhaa kama hizi zimesababisha vurugu ambapo watu wanne waliuwawa wiki iliopita wakati maafisa wa usalama walipowashambulia waandamanaji.

Mwandishi: Amina Abubakar/REUTERS/AFP

Mhariri: Elizabeth Shoo