1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Cameroon kusubiri matokeo siku 15

Admin.WagnerD8 Oktoba 2018

Tume ya Uchaguzi nchini Cameroon pamoja na waangalizi wa Umoja wa Afrika wamesema uchaguzi uliofanyika jana Jumapili ulikuwa wenye ufanisi kwa sehemu kubwa licha ya kukumbwa na makosa madogo madogo.

https://p.dw.com/p/36BQv
Kamerun Präsidentschaftswahlen l Anhänger der MRC
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 85 na kiongozi wa Afrika ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu, alikuwa na wapinzani saba katika uchaguzi huo ambao anapigiwa upatu kushinda. Huku raia wa Cameroon wakisubiri matokeo, serikali imetoa onyo dhidi ya kuchapishwa kwa matokeo yoyote kabla ya tangazo rasmi kutolewa na baraza la kikatiba, ambalo lina siku kumi na tano kumtangaza mshindi.

Zaidi ya waangalizi elfu saba walifuatilia uchaguzi huo ambapo wapiga kura milioni 6.6 walisajiliwa kushiriki. Kuliwepo na vurugu katika eneo la Kusini Magharibi na Kaskazini Magharibi ya nchi hiyo yanayozungumza Kiingreza, ambapo wanaotaka kujitenga waliwatishia wapiga kura. Baadhi ya waangalizi wanasema wapiga kura walijitokeza kushiriki uchaguzi katika maeneo hayo.

Kamerun Wahlen
Picha: Dr. Dirke Köpp

Kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo, kila kituo cha kupigia kura lazima kiwasilishe matokeo yake, baada ya kukaguliwa na Tume ya uchaguzi Elecam, kwa Mahakama ya Kikatiba ambayo ina jukumu la kutangaza matokeo rasmi yaliyojumlishwa katika muda wa siku kumi na tano.Mmoja wa raia wa nchini hiyo kwa jina Andre, anasema udanganyifu hauwezi kuepukwa na kwamba ni jambo la asili nchini Cameroon. "Tumezoea udanganyifu. Wanaposema inachukua siku kumi na tano kutoa matokeo ya uchaguzi, ina maana kwamba kuna udanganyifu. Siku kumi na tano kujumlisha matokeo ni ishara kuwa udanganyifu hauwezi kuepukika."

Matokeo katika mitandao ya kijamii

Baadhi ya matokeo yasiyokuwa rasmi kutoka vituo elfu 25 yalikuwa yameanza kusambazwa katika mitandao ya kijamii. Wagombeaji wa upinzani wamewashauri wafuasi wao kusimamia shughuli ya kuhesabu kura kuzuia udanganyifu ambao unaweza kumpendelea Rais Biya anayatazamia kuchaguliwa tena.

Mwanafunzi mmoja ambaye alishiriki uchaguzi huo kwa jina Raissa, anasema uchaguzi huo uliendeshwa kwa njia nzuri na hahisi kulikuwepo udanganyifu. "Hapana, hakuna udanganyifu. Kila kitu kilikwenda sawa. Hatukusikia kuhusu matatizo yoyote. Na iwapo yalikuwepo wanapaswa kuthibitisha. Kwa hivyo tunasubiri matokeo."

Kamerun Präsidentschaftswahlen l Maurice Kamto MRC
Kiongozi wa chama pinzani nchini Cameroon Movement for the Rebirth of Cameroon MRC, Maurice Kmeto (mwenye shati jekundu)Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Awali mmoja wa wagombeaji wa upinzani Maurice Kamto ambaye aliungwa mkono wakati wa mwisho mwisho na mgombeaji mwingine, alionya kuwa hatakubali matokeo yoyote yatakayokumbwa na udanganyifu. Shirika la habari la kitaifa nchini Cameroon limesema kwamba Waziri wa Serikali za Mitaa Paul Atanga Nji, aliwataka wanasiasa wote kuwajibika ili shughuli hiyo ikamilike vyema, sawa na ilivyoanza.

Kwa mujibu wa Kundi la Kitaifa kuhusu Migogoro, ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika maeneo yanayozungumza Kiingereza yamesababisha vifo vya raia 420, maafisa 175 wa idara za usalama na idadi isiyojulikana ya wanaotaka kujitenga.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/APE

Mhariri: Iddi Sessanga