Raia wa Burkina Faso waunga mkono Jeshi kuliongoza Taifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Raia wa Burkina Faso waunga mkono Jeshi kuliongoza Taifa

Huku wanadiplomasi wa matiafa ya magharibi wakiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa Burkina Faso, raia wa nchi hiyo wanaliunga mkono jeshi kuongoza mchakato wa mageuzi katika taifa hilo.

Huku baadhi ya wanadiplomasia wakiwa wameeleza wasiwasi wao kuhusu jukumu la jeshi katika siasa tangu maandamano yaliyomuangusha madarakani rais wa muda mrefu Blaise Compare mwezi Oktoba mwaka huu, ni Waburikabe wachache tu wenye wasiwasi mkubwa kuhusu jeshi kuendelea kuyalinda mapinduzi yao na kuruhusu mageuzi muhimu waliyoyadai.

Wakati kanali Isaac Zidda alipoyavua magwada yake ya kijeshi na kuvaa suti kuwa mwenyekiti wa mkutano wa kwanza wa baraza la mawaziri kama waziri mkuu wa Burkina Faso, huenda alitaka kutuma ujumbe kwa nchi za Magharibi na washirika wa barani Afrika. Ingawa watu kadhaa waliuwawa kwa kupigwa risasi wakati wa mapinduzi ya Burkina Faso, kanali Zida alizikonga nyoyo za waandamanaji wakati wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais alichokuwa akikiongoza kilipokataa kuufyetulia risasi umati wa watu waliokuwa wakiingia katika jengo la bunge.

Alishangiliwa kama shujaa alipowahutubia waandamanaji katika uwanja wa uhuru, kiasi cha kulinganishwa na shujaa wa mrengo wa shoto Thomas Sankara aliyeitawala Burkina Faso kati ya mwaka 1983 na 1987.

Burkina Faso Premierminister Isaac Zida 21.11.2014 Ouagadougou

Isaac Zida Waziri mkuu Burkina Faso

"Ukiona tunaendelea kufanya kazi na wanajeshi hawa leo, ni kwa sababu walifanya kazi yao ya kulinda badala ya kuwapiga risasi raia," alisema Michel Kafando, rais mpya wa mpito wa Burkina Faso, ambaye baraza lake lina mawaziri sita ambao ni maafisa wa jeshi.

"Watabaki na sisi kwa kuwa wamedhihirisha utiifu wao kwa raia. Vinginevyo tungetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe," akaongezeka kusema rais huyo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Ufaransa, France 24.

Zida analionyesha jeshi la Burkina Faso kama mlinzi wa mapinduzi. Anaahidi kufanya mageuzi pamoja na kuvichunguza visa vya rushwa na vifo vilivyotokea katika mazingira yasiyoeleweka wakati wa enzi ya Compaore.

Zida ameshawahi kuliambia taifa kwamba wizara ya sheria itakuwa na kibarua kikubwa na kigumu na itakuwa na jukumu muhimu wakati wa kipindi cha mpito.

Kuingia jeshi madarakani kulitokea kwa bahati mbaya. Viongozi wa upinzani wa Burkina walisita kutoa miito kutaka Campaore aondolewe madarakani hata katika wakati ambapo maandamano yalikuwa yakipamba moto kupinga jitihada zake za kuibadili katiba ili aweze kugombea tena wadhifa wa urais katika uchaguzi mwakani.

Mambo yalibadilika kwa haraka kuliko mahasimu wa Compaore walivyodhania. Baada ya Compaore kusitisha kura kuhusu mageuzi ya katiba, makundi ya watu waliandamana kuelekea ikulu yake na kumlazimisha ang'atuke. Katika makao makuu ya chama chake katika mji mkuu Ouagadougou, bia na chakula kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya sherehe baada ya mageuzi ya katiba kupitishwa, kililiwa na waandamanaji waliojawa na ghadhabu.

Burkina Faso ÜbergangsPräsident Michel Kafando

Michel Kafando Rais wa mpito Burkina Faso

"Viongozi wa kisiasa hawakuwa tayari. Vijana waliendeleza shinikizo na jeshi lilifanya vile watu walivyotaka," amesema Luc Marius Ibriga, profesa wa sheria na kiongozi wa jumuiya ya kiraia. "Tungependelea kuwa na serikali ya kiraia, lakini hii ndio hali halisi ya kisiasa Burkina Faso," akaongeza kusema profesa huyo.

Pascal Marie Iliboudo, mwanachama wa chama wa MPP, amesema anaunga mkono miito ya Zida kutafuta haki kwa uhalifu uliotendwa wakati wa utawala wa Compaore, lakini akasema kanali huyo hatakiwi kuruhusiwa kuzoweya utamu wa madaraka.

Profesa Ibriga amesema viongozi wa Burkina Faso hawakuelewa ushauri wa mabalozi wa nchi za kigeni waliosema Compaore alipanga kurefusha utawala wake wa miaka 27, lakini wakaingilia kati kuwashauri jinsi ya kusimamia kipindi cha mpito na kurejesha madaraka wa utawala wa kiraia.

Rinaldo Depagne, Mkuu wa shirika la Kimatiafa linaloshughulikia mizozo, ICG, kanda ya Afrika Magharibi, amesema yumkini kukatokea mivutano kati ya vyama vinavyotaka uchaguzi ufanyike haraka iwezekanavyo na makundi mengine yanayotaka mageuzi yapewe kipaumbele.

Serikali mpya ya Burkina Faso inakabiliwa na uhaba wa fedha huku athari za mapinduzi zikianza kuathiri uwekezaji na hazina za serikali kuanzia kodi hadi mauzo ya dhamana. Depagne amesema viongozi wanatakiwa waamue wanachotaka kukifanikisha.

Mwandishi: Nyamiti Kayora/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com