Radovan Karadzic asomewa mashtaka | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 31.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Radovan Karadzic asomewa mashtaka

Kiongozi wa zamani wa Wasabu wa Bosnia Radovan Karadzic amefikishwa mahakamani kusomewa mashtaka 11 juu ya mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na makosa dhidi ya binaadamu yanayomkabili.

Radovan Karadzic akifikishwa mahakamani na polisi

Radovan Karadzic akifikishwa mahakamani na polisi

Jaji aliyeongoza kikao cha mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani, ameanza kuhakikisha kwamba mtuhumiwa aliyekuwa mbele ya mahakama ni yeye Radovan Karadzic.

Baada ya kukamilisha utaratibu wa kumtambulisha mtuhumiwa kwa mahakama, umeanza ukurasa wa mashtaka yote ambayo yalitungwa mwaka 2000. Mwendeshamashtaka amemsomea historia ya majukumu yake kama kiongozi wa chama cha Kisabu katika Bosnia- Herzegovina ambayo ilikuwa sehemu ya Yugoslavia ya zamani, kwamba alikuwa kiongozi wa kisiasa na kiongozi wa majeshi na polisi katika Bosnia ambako katika vita vya kati ya mwaka 1992 na 1995, waislamu kiasi ya 8.000 waliuawa katika kijiji cha Sebrenica katika kile mahakama imekitaja mauaji ya kuangamiza jamii.Tuhuma nyingine ni kuwahamisha kwa nguvu watu kwa msingi wa kikabila na kuwateka nyara wafanyakazi na wanajeshi wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani na kuwanyanyasa wakaazi wa mji wa Sarajevo uliyokuwa umekaliwa na majeshi ya kisabu.

Kulingana na utaratibu wa kisheria kwenye mahakama hiyo, Radovan Karadzic anazo siku 30 yaani mwezi mzima kuanzia siku ya kwanza ya kufikishwa mahakamani ili kutoa hoja zake za utetezi. Hata hivyo pamoja na kuwa na haki hiyo ya kusubiri mwezi mzima, anayo pia haki ya kujibu moja kwa moja au kunyamanza kimya.

Radovan Karadzic ambae alikuwa peke yake bila wakili, amesema atajitetea mwenyewe na ameamua kutumia muda huo wa siku 30 kuyajibu mashtaka yanayomkabili.

Kabla ya kikao hicho kuanza kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague Uholanzi, wakili wa Radovan Karadzic Svetozar Vujacic aliyeko nyumbani mjini Belgrade, amewaambia waandishi wa habari mjini humo kwamba Karadzic atumia muda huo kusuka vizuri hoja zake.

Mwendeshamashtaka mkuu katika mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani Serge Brammertz, amewaambia waandishi habari mjini The Hague kwamba pamoja na kumsomea mashtaka Radovan Karadzic, wafanyakazi wa mahakama hiyo wamekuwa wakiirudia faili ya mashtaka ambayo ilitungwa mwaka 2000, kwa kuzingatia sheria mpya na ushadi mpya vile vile uliyotolewa katika kipindi hicho cha miaka minanne iliyopita.
 • Tarehe 31.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eo1C
 • Tarehe 31.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eo1C
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com