1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

Mtullya, Abdu Said17 Julai 2008

Kaazika maoni yao leo, wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya hatua ya kubadilishana wafungwa baina ya Israel na Hezbollah.

https://p.dw.com/p/EeI8
Wanajeshi wa Israel katika vita vya mwaka wa 2006 nchini Lebanon.Picha: AP

Magazeti  mengi ya Ujerumani leo yametoa  maoni yao  juu ya  kutekelezwa hatua  ya  kubadilishana wafungwa baina  ya  Israel  na  Hezbollah.

Mhariri  wa   gazeti  la   Dresdener Neueste Nachrichten  anasema  Israel imemwachia  muuaji  mkubwa  Samir Kuntar.  Mhariri  huyo  anasema kuachiwa kwa gaidi huyo  kunathibitisha ni kwa kiasi  gani serikali ya Israel inaweza  kushinikizwa. Gazeti hilo pia linasema  kuwa  hatua hiyo  pia inathibitisha  kuwa Hezbollah  ni  jumuiya yenye  uzito mkubwa kisiasa na kijeshi. Mhariri wa Dresdener Neueste Nachirichten  anaeleza katika  maoni yake kwamba  hakuna  anaeweza kuipuuza  Hezbollah.

Gazeti la Rhein Neckar pia linazungumzia  juu ya hatua hiyo ya kubadilishana  wafungwa baina ya Israel na Hezbollah.

Mhariri  wa gazeti  hilo  anauliza  vipi itawezekana  kuleta  amani katika  eneo ambapo upande fulani  unashingilia kifo kinachotokea   katika upande mwingine? Mhariri  huyo  anasema Mashariki  ya  Kati ni mahala  ambapo watoto  wa  kipalestina  wanageuzwa kuwa watu wenye itikadi kali  na  Israel. Ni vigumu kwa  Israel kukabiliana na uchokozi  uliopo sasa  bila ya kuchukua hatua za kijeshi.

Lakini gazeti la Rhein Neckar  linasema, kuwa siasa  ya kutoana macho na meno sasa haifai tena.Kinachotakiwa ni sera ya maridhiano kama jinsi  ilivyofanyika nchini  Afrika Kusini  na  Ireland.

Gazeti la Badische Zeitung  linauliza  jee nani ni mshindi  katika  mgogoro wa Mashariki  ya Kati ? 

Au nani  ameshindwa  katika  mgogoro huo? Gazeti hilo linasema  pande  zote zimeondoka na  majeraha   usoni. Yumkini  kiongozi wa Hezbollah  Hassan Nasrallah  anashingilia  ushindi kutokana  na kuachiwa  wafungwa  wa Hezbollah.  Lakini  ukweli  ni  kwamba kiongozi huyo anatoka nje ya maficho yake  kwa  nadra sana.   Mhariri  wa gazeti hilo pia  anakumbusha juu ya walebanon 1200 waliouawa  katika  vita vya  mwaka 2006. Gazeti  la Badische Zeitung  pia linasema  kwamba  Israel nayo  ilipata  funzo kubwa kutokana  na vita  hivyo. Mhariri  anahoji kuwa haikuwa lazima kwa  Israel kwenda vitani  ati  kwa sababu ya askari wake kuvamiwa mpakani na  wapiganaji wa Hezbollah.